Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa kimataifa wahitajika kuepusha mamilioni ya Wazimbabwe na janga la njaa:WFP

Mama akiwafundisha wanae katika wilaya ya Shamva nchini Zimbabwe wakati wamlipuko wa COVID-19.
WFP/Tatenda Macheka
Mama akiwafundisha wanae katika wilaya ya Shamva nchini Zimbabwe wakati wamlipuko wa COVID-19.

Msaada wa kimataifa wahitajika kuepusha mamilioni ya Wazimbabwe na janga la njaa:WFP

Afya

Zimbabwe ambayo tayari ina matatizo makubwa ya chakula kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na mdororo wa uchumi sasa janga la mlipuko wa virusi vya Corona unatishia kutumbukiza mamilioni ya watu wa nchi hiyo katika janga la njaa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP.

Katika taarifa iliyotolewa leo WFP inahitaji haraka msaada wa kimataifa wa dola milioni 130 kuweza kulisha taifa hilo la Afrika hadi mwezi Agosti kwa operesheni za dharura za chakula ili kuzuia mamilioni ya watu walio katika hatari nchini humo kuingia zaidi katika janga la njaa.

Kwa mujibu wa WFP tathimini iliyofanyika nchi nzima imeonyesha kwamba idadi ya Wazimbabwe ambao hawana uhakika wa chakula imepanda na kufikia watu milioni 4.3 kutoka watu milioni 3.8 mwishoni mwa mwaka jana.

“wakati tayari Wazimbabwe wengi wanahaha kuweka mlo mezani , mlipuko wa COVID-19 unahatarisha hali kubwa mbaya zaidi. Ni lazima tufanye kila tuwezalo kuzuia janga hili kuwa zahma kubwa” amesema Eddie Rowe mkurugenzi wa WFP nchini Zimbabwe.

 

Mfanyakazi wa shirika la mpango wa chakula duniani akizingatia nafasi wakati wa kugawa chakula wilaya ya Shamva nchini Zimbabwe.
WFP/Tatenda Macheka
Mfanyakazi wa shirika la mpango wa chakula duniani akizingatia nafasi wakati wa kugawa chakula wilaya ya Shamva nchini Zimbabwe.

Msaada unaotolewa na WFP

Msaada uliotolewa na WFP katika miezi ya karibuni umesaidia kupunguza njaa katika wilaya sita kati ya tisa zilizoorodheshwa mwishoni mwa kama jana kuwa ziko katika daraja la nne la dharura ya uhakika wa chakula.

 Sasa WFP inasema kiwango cha njaa katika wilaya hizo kimeshuka hata hivyo wilaya 56 kati ya 60 za nchi hiyo hivi sasa zimeelezewa kuwa katika mgogoro mkubwa wa chakula. WFP inazisaidia jamii ambazo ziko katika mgogoro na dharura kubwa ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

WFP inapanga kuwasaidia watu milioni 4.1 mwezi huu wa Aprili ingawa uhaba wa fedha umezuia kufikia lengo la kila mwezi tangu mwanzo wa mwaka huu. Mwezi Machi WFP imewafikia Wazimbabwe milioni 3.7 wasiojiweza.

Idadi ya walioathirika na njaa

Kwa mujibu wa shirika la WFP jumla ya watu wasio na uhakika wa chakula nchini Zimbabwe sasa I milioni 7.7 ambao ni nusu ya watu wote wa taifa hilo.

Dola milioni 130 zinazohitajika haraka na WFP ni sehemu ya msaada wa jumla wa chakula ambao unahitaji dola milioni 472 kulisaidia taifa hilo hadi Desemba.

Uzalishaji wa nafaka mwaka 2019 ulikuwa nusu ya ilivyokuwa mwaka 2018 na ni chini ya nusu ya mahitaji ya kitaifa. Wataalm wanatabiri kwamba mavuno yam waka huu wa 2020 yatakuwa mabaya zaidi.

Asilimia kubwa ya chakula cha Zimbabwe kinazalishwa na wakulima wa kawaida ambao wanategemea mvua pekee.

Mfumko wa bei ya vyakula shirika la WFP linasema wamelazimishwa wazimbabwe wengi kupunguza idadi ya milo, kuuza vitu vyao vya thamani kupata fedha za kununua chakula na kutumbukia katika madeni.

Limeongeza kuwa sasa janga la COVID-19 linatishia kufanya hali mbaya ya kiuchumi ya Zimbabwe kuwa mbaya zaidi na kuzusha janga la njaa likiathiri maisha ya watu wote wa mijini na vijijini.