Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujuzi tulioupata wakati wa Ebola tutautumia kupambana na COVID-19-Wauguzi DRC

Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo
UN Photo/Martine Perret
Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo

Ujuzi tulioupata wakati wa Ebola tutautumia kupambana na COVID-19-Wauguzi DRC

Afya

Wakati mlipuko wa ugonjwa Ebola ukielekea kufikia ukingoni nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, wahudumu wa afya waliopata mafunzo wakati wa janga hilo, hivi sasa wanatumia ujuzi walioupata, kuimarisha mfumo wa afya nchini humo ikiwa na kutumia uwezo huo kupambana na virusi vya corona, COVID-19.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linasema kama hakuna mgonjwa yeyote mpya atakayetokea, mlipuko wa sasa wa Ebola nchini DRC utatangazwa kufikia ukomo katikati ya mwezi huu wa Aprili, 2020. 

Wafanyakazi wa sekta ya afya nchini DRC walikuwa mstari wa mbele katika kupambana na Ebola. Walipokea mafunzo na vifaa kutoka WHO na washirika wake ili kuwasaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola, huku wakijilinda wao wenyewe kutoambukizwa.

Muuguzi Esperance Kavira Kavota ni mmoja wa wauguzi ambaye kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu amefanya kazi katika kituo cha kutoa tiba ya Ebola katika mji wa Beni, moja ya vitovu vya mlipuko wa Ebola. Na sasa kwa kuwa mlipuko wa Ebola unaelekea mwisho, amerejea kazini katika wodi ya wanawake wanaojifungua katika Hospitali ya Beni. Katova anaeleza uzoefu kama wenye kuleta msongo mwanzoni kutokana na kukutana kwao na wagonjwa ambao wameambukizwa,“hatukuwa na vitu vya kujikinga, tulikuwa tunavaa tu aproni za mpira, glovu na barakoa. Hivyo tu. Kisha muungano wa kimataifa wa hatua za tiba (ALIMA), na WHO wakaja. Mashirika yote waliweka nguvu yao pamoja na sasa tunafahamu jinsi ya kujitenga vizuri na kituo hiki cha Ebola kikajengwa.”

Uzoefu walioupata wahudumu hawa wa afya, pamoja na miundombinu ya Ebola iliyojengwa inaweza kutumika kuimarisha mfumo wa afya na kupambana na milipuko mingine kama Ebola. Bi Kavota anaendelea,“kabla ya mlipuko huu wa Ebola, hatukuwa na mafunzo ya kuzuia na kudhibiti maambukizi au mafunzo  kwa ajili ya kushughulikia waliofariki au hata ufahamu kuhusu tiba mahususi ya Ebola. Lakini baadaye tulipokea mafunzo kuhusu virusi vya Ebola na tiba yake. Wageni wengi walikuja hapa na uzoefu wao na wakatufundisha. Walitupatia vifaa ambavyo hatukuwa tumevitumia kabla, na mbinu nyingi mpya. Zilitusaidia. Katika tukio la mlipuko mwingine, tutaweza kuushughulikia kwa wakati unaofaa.”

Kavota anasema wakati huu ambao Ebola inaelekea ukingoni, wauguzi kama yeye watakuwepo wakati wote kuhudumia hospitali kwa uwezo wao wote.