UN na wadau Somalia watoa kipaumbele cha kukabiliana na COVID-19

7 Aprili 2020

Umoja wa Mataifa na washirika wake wa masuala ya kibinafdamu nchini Somalia wanaweka mipango na vipaumbele vipya ili kusaidia taifa hilo la Pembe ya Afrika katika maandalizi na hatua za kupambana na virusi vya Corona COVID-19.

Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Somalia imeorodhesha wagonjwa 7 waliothibitishwa na hakuna kifo chochote cha COVID-19

Imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufunga shule zote , kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa na kusitisha safari za ndege za kitaifa na kimataifa.

Shirika la Umoja wa Mataia la masuala ya kibinadamu na kuratibu misaada ya dharura OCHA linasema hatua zinazochukuliwa na jumuiya ya misaada ya kibinadamu zinajikita katika kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo na kuzuia maambukizi mapya. 

Pia juhudi zinaendelea kuimarisha ufuatiliaji , hatua za haraka na upimaji ili kuwezesha kubaini , kupima na kufuatilia washukiwa wote wa ugonjwa huo wa Corona.

Mashirika yanashirikiana na serikali

OCHA inasema mashirika ya misaada ya kibinadamu yanashirikiana na serikali kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, kuanzisha vito ambavyo wanaweka watu wanaoumwa kujitenga na wengine, kupeleka wahudumu wa afya katika ameneo ambayo watu wanaingilia na kuhakikisha hatua za kuzingatia usafi.

Hadi sasa wahudumu wa afya wameshapelekwa katika vituo vyote 23 vilivyotengwa na serikali kama ni sehemu za kuingilia ikiwemo viwanja vine vya kimataifa vya ndege Moghadishu, Garowe, Bossaso na Hargeisa. Na mipaka na majirani zao Ethiopia na Kenya imefungwa kuzuia watu kuvuka na kuingia.

Changamoto na hofu

Yang Yi
Madaktari wakimpa huduma mgonjwa wa virusi vya corona, COVID-19

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wasiwasi ni ukweli kwamba katika baadhi ya sehemu idadi ya wahudumu wa afya ni wawili kwa watu 100,000 ukilinganisha na viwango vya kimataifa vinavyotaka wahudumu 25 kwa watu 100,000.

Na vituo vya afya vilivyo na vifaa vinavyohitajika kukabiliana na COVID-19 ni chini ya asilimia 20.

Pia kuna hofu ya hatari ya maambukizi kusambaa haraka kwa sababu na msongamano katika makazi duni na kukosekana kwa kuhuduma za msingi kama maji na usafi.

WFP imeweka mikakati

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limesema limeweka mipango ya opresheni zake nchini Somalia ambayo inatoa kipaumbele cha mahitaji ya haraka miongoni mwa watu wasiojiweza nchini humo ili kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa endapo janga hilo litakuwa baya zaidi.

Shirika hilo limeonya kwamba mlipuko wa COVID-19 Somalia unaweza kuongezewa chachu kirahisi kutokana na hali tete ya uhakika wa chakula nchi nzima.

Miongoni mwa mambo ambayo WFP inayafanya kusaidia kukabiliana na hali hiyo ni kutoa kipaumbele katika msaada wa chakula wa kuokoa Maisha kwa watu wasiojiweza na mwezi huu wa Aprili itatoa mgao wa chakula wa miezi miwili au fedha taslim saw ana mgao huo kwa watu zaidi ya milioni moja ambao wameathirika na kutokuwa na uhakika wa chakula kote Somalia.

Kuna wakimbizi wa ndani milioni 2.6 nchini Somalia ambao amba wana fursa ndogo sana ya huduma za afya au hawana kabisa na watu milioni 1.4 hawana uhakika wa chakula na wenginge wanaoishi katika maeneo yaliyoathirika na nzige na yenye ukame.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud