Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi kwenye utoaji huduma dhidi ya COVID-19 utaleta janga zaidi- Wataalamu

Mkimbizi wa ndani ambaye anarejea nyumbani kwa hiari Bentiu, Sudan Kusini kipimwa homa.
UN Photo/Isaac Billy
Mkimbizi wa ndani ambaye anarejea nyumbani kwa hiari Bentiu, Sudan Kusini kipimwa homa.

Ubaguzi kwenye utoaji huduma dhidi ya COVID-19 utaleta janga zaidi- Wataalamu

Haki za binadamu

Kikosi kazi cha waatalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye asili ya Afrika, kimetaka kuwepo na uwiano na usawa wa makundi mbalimbali ya binadamu wakati wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, la sivyo utoaji wa huduma kwa misingi ya rangi unaweza kusababisha vifo zaidi.

Wito huo umo kwenye taarifa ya wataalamu hao wanaojitika kwa haki za watu walio na asili ya Afrika, taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi ikisema kuwa ubaguzi wa kimfumo katika utoaji  huduma unaleta matokeo ya kibaguzi na vifo zaidi na idadi ya wagonjwa miongoni mwa watu wenye asili ya Afrika.

Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho Ahmed Reid amesema, “licha ya hatua mujarabu zilizochukuliwa, serikali bado hazijatambua athari mahsusi za kiafya zinazokabili watu wenye asili ya kiafrika au jinsi ubaguzi wa rangi na upendeleo kwa misingi ya rangi vinaweza kuchochea sera hiyo.”

 Wataalamu hao wa haki za binadamu wamesisitiza kuwa tatizo linigne ni ukosefu wa uwakilishi katika ngazi ya juu wakisema kuwa, “hii inazuia kusambaza utaalamu na ulinzi kwa mahitaji ya watu wenye asili ya Afrika wakati wa utekelezaji wa hatua dhidi ya COVID-19.”

Wataalamu hao wamesisitiza kuwa serikali zinapaswa kuchunguz jinsi gani upendeleo wa aina huo bila mwongozo wowote unaweza kufanya janga la COVID-19 kuwa kubwa zaidi kwa baadhi ya watu wa rangi fulani wakiongeza kuwa, “tayari ambako kwenye data zilizonyumbuliwa, tofauti za huduma kwa misingi ya rangi ya watu ni dhahiri.”

 Mathalani wamesema kuwa, “hatua zinazoonekana usoni kuwa haziegemei upande wowote zinaweza kuruhusu au kuchochea ubaguzi wa rangi. Kwa mantiki kwamba hadi sasa hakuna hatua za kulinda au kujikita katika utoaji huduma za afya kwa kuzingatia hatari wanazokabiliwa nazo watu wa makundi fulani ikiwemo waafrika na wenye ulemavu.”

Wamesisitiza kuwa mazingira ambamo kwayo watu wa asili ya Afrika wanafanya kazi au kwenye jela wanamofungwa, kunahatarisha zaidi maisha yao katika kuambukizwa virusi vya Corona.

Ni kwa mantiki hiyo, wataalamu hao wamesisitiza kuwa suala kwamba wafanyakazi wa afya na wahudumu mashinani waliozidiwa uwezo wanapaswa kupata mwongozo zaidi ikiwemo kuwasilisha data zilizonyambuliwa ili kuhakikisha kuwa kuna huduma zenye uwiano.

Ameongeza Bwana Reid kuwa “serikali zinazotumia janga la COVID-19  kusitisha au kupunguza haki za kibinadamu zinazotolewa kwa misingi ya upendeleo chanya zinakwamisha watu wenye asili ya kiafrika na hatua hizo zitadumu zaidi hata baada ya janga la Corona.”

 Hata hivyo kikundi kazi hicho kimekaribisha hatua za COVID-19 lakini kimesihi serikali kutambua udharura wa haki za binadamu na kuhakikisha huduma za elimu, afya, intaneti zinapatikana kwa watu wote na kwa nyakati zote.