Jumuiya ya michezo yakabiliwa na changamoto kubwa sababu ya COVID-19 :UN

6 Aprili 2020

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya michezo kwa maendeleo na amani , Umoja wa Mataifa umesema jumuiya ya kimataifa ya michezo inakabiliwa na changamoto kubwa wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 kwa watu wengi kushindwa kujumuika katika michezo mbalimbali na pia kufanya mazoezi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mlipuko wa COVID-19 unasambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali na hatua za kujitenga kuepuka mikusanyiko zimekuwa ndio maisha ya kila siku ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.

Hatua hizo zimesababishwa vituo vya michezo, vituo vya kufanyia mazoezi, viwanja vya michezo, mabwawa ya umma ya kuogelea, vituo vya kujifunza muziki na maeneo ya watoto kwenda kucheza kufungwa..

 Na hii inamaanisha kwamba “wengi wetu hatuwezi kushiriki mazoezi ya viungo iwe mmoja mmoja au kwa vikundi vya michezo mbalimbali, au shughuli zozote za mazoezi ya viungo, wala kuangalia mashindano ya michezo moja kwa moja.”

Umesema Umoja wa Mataifa ukiongeza kwamba na matokeo yake “jumuiya ya kimataifa ya michezo inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi mbalimbali kote duniani kupambana na COVID-19.”

Hata hivyo katika siku hii Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba hatua zote hizo hazimaanisi kwamba “sasa ndio tuache kufanya mazoezi ya viungo kabisa au tuache mawasiliano na makocha, wachezaji wenzetu, wakufunzi na mashabiki wenzetu wa michezo ambao sio tu kwamba wanatusaidia kuhakikisha tuko vyema kiviungo bali pia kijamii.”

Shirika la afya la umoja wa Mataifa WHO linapendekeza dakika 150 ya mazoezi ya wastani au dakika 75 za mazoezi makali kwa wiki au kufanya vyote.

WHO imesema kuna njia mbalimbali za kuhakikisha watu wanajishuhulisha kiviungo wakati huu wa COVID-19 ikiwemo kutumia nyenzo za bure mtandaaoni na hivyo inawachagiza watu wa rika zote kuhakikisha wanafanya mazoezi ya aina moja au nyingine wakati huu mamilioni ya watu wakisalia majumbani.

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa michezo ina uwezo wa kubadili dunia, ni haki ya msingi, nyenzo muhimu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuchagiza malengo ya maendeleo endelevu, amani, mshikamano na kuheshimiana.

Siku ya kimataifa ya michezo kwa ajili ya maendeleo na amani huadhimishwa kila mwaka Aprili 6.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter