Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lapitisha azimio la mshikamano duniani kutokomeza virusi vya Corona

Mkazi wa jiji la New York, nchini Marekani akiwa amevaa barakoa kujikinga dhidi ya virusi vya Corona, COVID-19.
UN Photo/Loey Felipe
Mkazi wa jiji la New York, nchini Marekani akiwa amevaa barakoa kujikinga dhidi ya virusi vya Corona, COVID-19.

Baraza Kuu lapitisha azimio la mshikamano duniani kutokomeza virusi vya Corona

Afya

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio la kuonesha mshikamano ya vita dhidi ya virusi vya Corona au COVID-19.
 

Azimio hilo namba A/74/L.52 limepitishwa katika mkutano uliofanyika kwa njia ya video wakati huu ambao mikutano yote ya Umoja wa Mataifa inafanyika kwa njia ya video kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona.

Nyaraka ya azimio hilo iliyochapishwa kwenye wavuti wa Baraza Kuu imesema azimio linazingatia tishio la virusi hivyo kwa afya ya binadamu, virusi ambavyo vinaendelea kusambaa duniani kila uchao.

“Kwa kutambua madhara yasiyo ya kawaida ya virusi vya Corona ikiwemo kutibua chumi za jamii, pamoja na safari na biashara, na madhara yake katika mbinu za watu kujipatia kipato, na pia kutambua kuwa janga hilo limeathiri zaidi watu maskini zaidi duniani,” imesema nyaraka hiyo yenye kurasa mbili.

Mitaa katika mji wa Bethlehem kwenye eneo la Palestina linalokaliwa ikiwa wazi kutokana na watu kuwa karantini tangu kuanza kwa mwezi Machi kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya corona.
Lubna Kharoufe
Mitaa katika mji wa Bethlehem kwenye eneo la Palestina linalokaliwa ikiwa wazi kutokana na watu kuwa karantini tangu kuanza kwa mwezi Machi kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya corona.

Azimio hilo limetambua pia dhima kuu ya mfumo wa Umoja wa Mataifa katika kuchagiza na kuratibu hatua za kimataifa za kudhibiti na kutokomeza virusi vya Corona sambamba na kutambua jukumu muhimu la shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO katika kuongoza juhudi za kukabiliana na virusi hivyo hatari ambavyo tarehe 29 mwezi Januari mwaka huu vilitangazwa kuwa tishio la afya ya umma duniani.

Baraza Kuu limekaribisha wito wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa wa kushughulikia dharura hiyo ya kimataifa na kujikita pia katika hatua za kukabili athari zake kiuchumi na kijamii huku hakikisho likitakiwa kuwa, “mbinu endelevu za kujikwamua na mbinu ziwe jumuishi.”

Kwa kutambua umuhimu wa mshikamano wa wadau wote katika kufanikisho hatua hizo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na mambo mengine linapigia chepuo mshikamano wa kimataifa na dhima kuu na ya msingi ya Umoja wa Mataifa na mashirika yake katika kudhibiti COVID-19.

“Tunasisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu katika kukabili virusi na kusiwepo na ubaguzi wowote, chuki dhidi ya wageni. Pia salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza ndugu na jamii na kutakia ahueni ambao bado wanahaha kunusuru maisha yao,”  limesema azimio hilo ambalo miongoni mwa nchi zilizounga mkono ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.

Baraza pia limeonesha matumaini yake kuwa janga hili la sasa la aina yake linaweza kupunguzwa au kudhibitiwa kwa mafanikio makubwa kupitia uongozi na ushirikiano endelevu wa kimataifa na hivyo limetoa wito kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa, chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, ufanye kazi na wadau wote husika ili kuhamasisha hatua za pamoja na hatimaye kukabili madhara ya kiuchumi, kijamii na kifedha kwa jamii zote.