Hofu ya maambukizi ya COVID-19 yasababisha soko la Sakure kufungwa nchini Sudan Kusini

2 Aprili 2020

Soko la kila wiki huko Sakure, karibu na mpaka kati ya Sudani Kusini na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC limefungwa kama sehemu ya juhudi za Serikali ya Sudani Kusini kudhibiti tishio la kimataifa la virusi vya corona au COVID-19

Soko hilo lilikuwa na shuhguli nyingi kila Ijumaa huku wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili wanakutana na kubadilishana bidhaa, lakini, serikali ya Sudani Kusini hivi karibuni imetangaza kufungwa kwa mipaka yake na nchi jirani. Na hatua hiyo imesababisha soko kufungwa pia.

Timu kutoka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS walitembelea eneo hilo kuangalia hali ya usalama na haki za binadamu na kufuatilia kurejea numbani na kujumuishwa kwa watu waliokimbia makwao pia shughuli za kibiashara mpakani.

Wafanyabiashara wanahisi athari za hatari inayotokana na virusi na kufungwa kwa mipaka katika kujaribu kuizuia kuwasili katika nchini ambayo tayari inapambana kujikwamua kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano. Venasio Sinoyosa ni Afisa wa Kliniki, Kituo cha Huduma ya Afya ya msingi cha Sakure

 

"Linapokuja suala la virusi vya corona, ikiwa litatufikia, nina uhakika watu wengi wataathirika kwa sababu hivi sasa hakuna uchunguzi hapa. Tunatoa uchunguzi kwa ajili ua ugonjwa wa Ebola tu. Labda uchunguzi utaanza baadaye, hatuna uhakika. Mpaka umefungwa, ndio, lakini kuna barabara nyingi ndogo za mkato ambapo watu wanaweza kupita na kwenda Kongo, Wakongo pia waje hapa."

Jamii nyingi zinazozunguka eneo hili la mpaka zinategemea soko hili la kila wiki kwa hivyo wafanyabiashara wanateseka kwa sababu ya kufungwa kwake.George Bol, ni mfanyabiashara wa Sudan Kusini

"Ninakuja hapa kila Ijumaa na chumvi na sabuni nauza kwa wakongo. Natumia pesa kununua unga, mafuta na mchele ambao mimi huchukua nyumbani kwa watoto wangu. Hii imekuwa kawaida yangu kila wiki lakini sasa itakuwa ngumu kwangu kulisha familia yangu. Hivi sasa, sina chochote nyumbani. Nilitamani kupata vitu vichache hapa leo.”

Lilian Sundry,mchuuzi kutoka Sudan Kusini pia, anaelekea nyumbani mikono mitupu, ingawa anasema anafurahi kupata wakati wa kulea watoto wake.

"Ni kweli inatuathiri kwa sababu tunategemea soko hili. Mimi huja hapa kununua mafuta ya mitende na kuiuza katika kijiji chetu. Hii imekuwa ikinisaidia. Lakini sasa na ugonjwa huu, hakuna kitu tunaweza kufanya. Lazima nirudi nyumbani na kutunza watoto wangu. "

Sudani Kusini kwa sasa ni moja wapo ya nchi chache barani Afrika ambazo hazina kesi yoyote ya visa vya COVID-19.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter