Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mpishi Ron Pickarski akikatakata mboga jikoni kwake Boulder Colorado

COVID-19 ikitikisa, mlo uwe vipi?

©FAO/Benjamin Rasmussen
Mpishi Ron Pickarski akikatakata mboga jikoni kwake Boulder Colorado

COVID-19 ikitikisa, mlo uwe vipi?

Afya

Wakati wazazi wengi wanatafuta milo iliyokwishapikwa tayari na vyakula vya kusindikwa kama njia ya haraka na ya bei nafuu ya kulisha familia, kuna njia mbadala rahisi, za bei nafuu na zenye afya  hasa wakati huu wa ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19

Mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, umebadili mwenendo wa maisha kwa familia duniani kote. Shule zimefungwa, wazazi wanafanyia kazi nyumbani huku wakilea watoto wao. Kuwaza mlo gani wa asubuhi, mchana au jioni ni changamoto nyingine. Hofu ilipotanda vyakula navyo upatikanaji umepungua, kwa waliopoteza ajira, ununuzi wa vyakula nao ni shida. Je wazazi wafanye nini? Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limekuandalia dondoo 5 zinazoweza kufungua njia.

Dondoo 5 za mlo wenye virutubisho kwa zama za sasa za COVID-19

Wanawake nchini Morocco wakipakia matunda katika makasha kwa ajili ya biashara.
FAO/Alessandra Benedetti
Wanawake nchini Morocco wakipakia matunda katika makasha kwa ajili ya biashara.

1.  Ulaji wa matunda na mboga

Kununua, kuhifadhi na kupika mboga zisizosindikwa kunaweza kuwa vigumu hasa wakati huu wa kutotembea hovyo, tena pale wazazi wanaposhauriwa kupunguza idadi ya safari nje ya nyumba. Lakini kila inapowezekana, ni muhimu kuhakikisha watoto bado wanapata matunda na mboga katika mlo wao.
Wakati wowote inapowezekana kupata mazao yasiyosindikwa, fanya hivyo. safi, fanya hivyo. Pamoja na kwamba mazao hayo yanaweza kuliwa, matunda na mboga pia zinaweza kuhifadhiwa kwenye jokofu na kuhifadhi virutubishi na ladha yao zaidi. Kutumia kiasi kikubwa cha mboga kutoka mashambani kwa ajili ya kupika supu, michuzi au vyakula vingine, hufanya vidumu zaidi na kutoa chaguzi nyingi za vyakula kwa siku za usoni. Aina hiyo ya mlo inaweza kuwekwa kwenye barafu ikaganda na kupashwa moto haraka kadri inavyohitajika.


2. Ukikosa mazao yasiyosindikwa, yale ya makopo ni mbadala 

Mazao ya kutoka shambani ambayo hayajasindikwa kila wakati ni chaguo bora, lakini wakati ni adimu kuna vitu mbadala ambavyo ni rahisi kuhifadhi na kuandaa.

Maharagwe na dengu za makopo yana virutubisho vingi na huweza hifadhiwa kwa miezi au hata miaka, na vinaweza kujumuishwa katika mlo kwa njia nyingi. Samaki wa kusindikwa kwenye kopo na mafuta kama dagaa, samoni na wengineo wana protini nyingi, vitamini na madini. Hivi huweza liwa hata vikiwa na baridi kwenye mkate, kachumbari au tambi au kupikwa kama sehemu ya mlo wa moto.
Mboga za makopo, kama vile nyanya, huwa na kiwango kidogo cha vitamini kuliko nyanya ambazo hazijasindikwa, lakini ni mbadala bora pindi nyanya za kawaida au zilizogandishwa zinapokuwa adimu kupata.

Maharagwe makavu ni lishe bora. Hapa ni sokoni , Jamhuri ya kidemokrasia ya COngo, DRC.
©FAO/Olivier Asselin
Maharagwe makavu ni lishe bora. Hapa ni sokoni , Jamhuri ya kidemokrasia ya COngo, DRC.


Mazao ya kukaushwa kama vile aina za maharagwe, kunde, choroko, au nafaka kama vile mchele, kusikusi au kinoa nayo pia yana virutubisho, huhifadhika kwa muda mrefu, yana ladha, bei nafuu pia. Nafaka ya ngano ukipika kwa maziwa au maji nayo huweza kuwa mbadala mzuri wa kifungua kinywa na unaweza kuongeza maziwa ya mgando, matunda au zabibu kavu. 

3. Hifadhi vitafunwa vyenye afya

Mara nyingi watoto huhitaji vitafunwa mchana mara moja au mara mbili. Badala ya kuwapatia peremende au vitafunwa vyenye chumvi wapatie vile vyenye afya kama vile jamii ya karanga, jibini, maziwa ya mgando yasiyoongezwa sukari, matunda hata yale ya kukaushwa, mayai ya kuchemsha au aina nyingine za vitafunwa vya kiasili. Vyakula hivi vina lishe, vinashibisha na husaidia kujenga tabia ya kula vyakula vyenye virutubisho maishani. 

4. Punguza vyakula vya kusindikwa

Wakati mazao yasiyosindikwa yanaweza yasipatikane kila wakati, jaribu kupunguza manunuzi ya vyakula vilivyosindika. Vyakula vilivyokwishapikwa, vitafunwa vilivyoko kwenye makasha mara nyingi huwa na mafuta mengi, sukari na chumvi. Ikiwa unanunua vyakula vya kusindikwa, angalia lebo na ujaribu kuchagua vyenye virutubishi na viambato vyenye afya. Jaribu pia kuzuia vinywaji vyenye sukari na badala yake unywe maji mengi. Kuongeza kwenye maji vitu kama vile mboga na matunda kama limao na ndimu, au vipande vya ni njia nzuri ya kuongeza ladha ya ziada.

 

5. Mapishi ya vyakula na mlo wa pamoja kwenye familia liwe jambo la furaha na utaratibu wako wa kifamilia

Kupika na kula pamoja ni njia nzuri ya kuunda mfumo wenye afya, kuimarisha utangamano wa familia na kujenga furaha. Kadri uwezavyo, shirikisha watoto katika maandalizi ya chakula - watoto wadogo wanaweza kusaidia kusafisha au kupanga vyakula. Watoto wakubwa wanaweza kuwa na majukumu makubwa zaidi na kusaidia kuandaa meza. Jaribu kadri uwezavyo kuzingatia muda wa mlo wa familia. Muundo na utaratibu kama huu unaweza kusaidia kupunguza wasiwasi kwa watoto katika zama za sasa za msongo.

Huko Montevideo nchini Uruguay, Chloe (kulia) akiwa na baba yake wakiandaa mlo.
UNICEF/UN0343152/Pazos
Huko Montevideo nchini Uruguay, Chloe (kulia) akiwa na baba yake wakiandaa mlo.