Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufungwa kwa shule kulikosababishwa na COVID-19 kutawaathiri vibaya sana wasichana-UNESCO

Nchi zilizoendelea kama Marekani, watoto wanaendelea na masomo kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona
© UNICEF/Lisa Adelson
Nchi zilizoendelea kama Marekani, watoto wanaendelea na masomo kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona

Kufungwa kwa shule kulikosababishwa na COVID-19 kutawaathiri vibaya sana wasichana-UNESCO

Utamaduni na Elimu

Kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, COVID-19 kulazimisha kufungwa kwa shule katika nchi 185 duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO kwa kushirikiana na shirika la Plan International limeonya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa idadi ya watoto watakaoacha shule suala ambalo litawaathiri zaidi wasichana wadogo na hivyo kuongeza pengo la jinsia katika elimu na hivyo kusababisha kuongezeka kwa hatari zaidi unynyasaji wa kingono, mimba za utotoni na ndoa za kulazimishwa na pia zile za mapema.

Taarifa hiyo imesema kati ya jumala ya watoto wote walioandikishwa na kujiunga shuleni duniani kote, UNESCO inakadiria kuwa zaidi ya asilimia 89 hivi sasa wako nje ya shule kwasababu ya COVID-19. Hii inawakilisha sawa na watoto bilioni 1.54 na vijana waliojiunga na shule au vyuo vikuu wakiwemo wasichana 743.

Aidha UNESCO inasema zaidi ya wasichana milioni 111 ya hawa wanaishi katika nchi zinazoendelea ambako kupata elimu tayari ni kizungumkuti. Katika nchi hizo kuna ufukara, hali mbaya ya uchumi na kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika elimu. Mathalani nchini Mali, Niger na Sudan Kusini, nchi tatu ambazo zinatajwa kuwa na idadi ndogo ya udahili na wasichana wanaohitimu masomo, kufungwa kwa shule kumewalazimisha wasichana zaidi ya milioni nne kuwa nje ya shule.

 

Kwa wasichana ambao wanaishi katika kambi za wakimbizi au ambao ni wakimbizi wa ndani, kufungwa kwa shule, litakuwa tatizo kubwa zaidi kwasababu tayari wako katika hali mbaya. Wasichana wakimbizi katika ngazi ya sekondari ni nusu ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

“Wakati wasichana wengi wataendelea na masomo baada ya shule kufunguliwa, wengine hawatarejea. Suala la kushughulikia elimu linatakiwa kutoa kipaumbele mahitaji ya wasichana mabinti ambao wako katika hatari ya kurejesha nyuma hatua za miaka ishirini ambazo zimeshapigwa kwa ajili ya elimu ya wasichana.” Imesisitiza taarifa hiyo.