MONUSCO na harakati za kudhibiti kuenea kwa COVID-19 nchini DRC

1 Aprili 2020

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako idadi ya wagonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ambao wamethibitishwa hadi leo hii ni 109 huku 8 (wanane) kati yao tayari wamefariki dunia, Umoja wa Mataifa umechukua hatua kuunga mkono hatua za serikali za kudhibiti kusambaa zaidi kwa virusi hivyo miongoni mwa wananchi wanaowahudumia na wafanyakazi wake.

Mathalani ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umechukua tahadhari hizo na baadhi ya hatua ni  kupunguza doria, kufuta safari zisizo za lazima ndani ya nchi, kufanya mikutano muhimu kwa kutumia teknolojia ya video ili kupunguza hatari zaidi.

 

Aidha timu ya matabibu kutoka MONUSCO imejiandaa na inafuatilia hali kwa karibu huku wakielezea kile wanachofanya kama anavyofafanua Sajini Ibrahim,  mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania.

"Tunanawa mikono kwa ajili ya kuweza kujikinga kutokana na Corona, lakini hatukuanza sasa ila wakati wa mlipuko wa ebola kwa hiyo kumekuwa na mwendelezo kwa ajili ya kuweza kujikinga na pia tunazingatia namna ya kusalimiana kwa kutumia miguu na kuwa mbali. Kwani kunawa mkono ndio msingi katika kujikinga kutokana na korona ukizingatia sehemu mbali mbali ambazo mikono inagusa."

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud