UNHCR yaunga mkono mashinani harakati za kukabili COVID-19

31 Machi 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limeweka bayana jinsi operesheni zake zinavyoendelea mashinani kusaidia harakati za kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 sambamba na kuepusha kuenea zaidi kwa virusi hivyo vilivyokwishasambaa katika nchi 199 duniani.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amenukuliwa katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa Geneva, Uswisi hii leo akisema kuwa licha ya gonjwa hilo kuwasababisha kurekebisha operesheni zao, wanafanya kila juhudi kusaidia na kulinda wakimbizi kadri wawezavyo katika mazingira magumu ya sasa.

 

“Kipaumbele chetu kikuu kwenye janga hili la COVID-19 ni kuhakikisha watu tunaowahudumiwa wanajumuishwa katika mipango ya hatua dhidi ya gonjwa hilo na wanapatiwa taarifa sahihi huku tukiunga mkono na kusaidia hatua za serikali kadri inavyohitajika,” amesema Bwana Grandi.

Tarehe 26 mwezi huu wa Machi, UNHCR ilitoa ombi la dola milioni 255 ikiwa ni sehemu ya ombi la Umoja wa Mataifa ili kujikita katika vipaumbele mahsusi vya kitaifa vinavyohitaji usaidizi.

UNHCR inasema kuwa ijapokuwa idadi ya wakimbizi walioambukizwa virusi vya Corona bado ni ndogo zaidi ya asilimia 80 ya wakimbizi duniani na wakimbizi wa ndani wanaishi kwenye nchi za kipato cha chini, ambazo nyingi zao zina mifumo dhaifu ya afya, maji, huduma za kujisafi na hivyo zinahitaji msaada wa haraka.

Bwana Grandi amesema, “wakimbizi wengi wanaishi kwenye kambi zenye msongamano au kwenye maeneo maskini mijini bila huduma za kujisafi, WASH, afya, na huduma za kinga kwenye maeneo hayo ni kipaumbele.”

Tunagawa sabuni na tunaelimisha wakimbizi na wenyeji

Ni kwa kuzingatia hali hiyo, hivi sasa UNHCR imechukua hatua kama vile kuimarisha huduma za afya na mifumo ya maji na kujisafi au WASH, kusambaza sabuni na kuhakikisha maji tiririka yanapatikana.

Shirika hilo pia linasaidia serikali katika harakati za kuepusha maambukizi na huduma za afya kupitia misaada ya vifaa vya matibabu pamoja na kusambaza vifaa vya makazi, msaada wa fedha taslimu kusaidia kupunguza makali ya kiuchumi na kijamii ya COVID-19 na kufuatilia kuhakikisha haki za waliofurushwa zinaheshimiwa.

Mathalani nchini Bangladesh, UNHCR imeanza kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa vituo vya afya kwenye kambi za wakimbizi warohingya ambako wakimbizi 850,000 wanaishi katika kambi zenye msongamnao.

UNHCR inasema zaidi ya wafanyakazi 2000 wa kujitolea wanafanya kazi na viongozi wa kijamii na kidini kuelimisha mbinu muhimu za kujikinga na virusi vya Corona ambapo elimu hiyo inatolewa kwa njia ya radio, video, mabango na vipeperushi.

Nchini Jordan, kazi ya kupima joto inafanyika katika lango la kambi ya Za’atari na Azraq na kampeni za uhamasishaji na uelimishaji nazo zinafanyika huku umeme ukipatikana na maduka makubwa ya vyakula na bidhaa muhimu yanatoa huduma kwa muda mrefu ili kuepusha msongamano.

Huko Ethiopia na Uganda vituo vya kunawa mikono kwa sabuni, kupima joto vimewekwa katika malango ya kuingia vituo vya mpito kwa wakimbizi ilhali huko Sudan, UNHCR imesambamba zaidi ya sabuni 260,000 kwa wakimbizi wa ndani na wenyeji wao.

Mikakati ya kuzuia Corona pia imechukuliwa na UNHCR kwenye kambi za wakimbizi wa ndani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Burkina Faso ikiwemo kuweka vituo vya kunawa mikono, mgao wa sabuni na kampeni za kuelimisha umma.

Kamishna Mkuu Grandi amesema wataendelea kupanua wigo wa huduma zao lakini kutekeleza hilo, wanahitaji msaada wa fedha.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter