COVID-19 yasababisha Olimpiki kusogezwa mwaka mmoja mbele, sasa kuchezwa 2021

31 Machi 2020

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC na Kamati ya kimataifa ya Paralimpiki IPC au Olimpiki ya watu wenye ulemavu, kwa pamoja kamati ya maandalizi ya Tokyo 2020, Serikali ya mji wa Tokyo na serikali ya Japani wametangaza kuwa kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19, sasa michezo ya Olimpiki iliyokuwa ifanyike mwaka huu mjini Tokyo, itafanyika mwaka ujao wa 2021.

Tangazo hili la tarehe mpya limekuja takribani wiki moja baada ya kutangazwa kuahirishwa kwa michezo hiyo.

Mamlaka hizo zimetangaza kuwa michezo ya Olimpiki itafanyika kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 8 Agosti mwakani, wakati ile ya watu wenye ulemavu ikifanyika kuanzia tarehe 24 Agosti hadi Septemba mwaka huo wa kesho 2021.

Makubaliano ya tarehe mpya yamefikiwa wakati wa mkutano kwa njia ya simu yaloiyofanywa kati ya Rais wa IOC Thomas Bach, Rais wa Tokyo 2020 Mori Yoshirō, Gavana wa Tokyo Koike Yuriko na Waziri wa Olimpiki na Paralimpiki Hashimoto Seiko.

Tarehe mpya ni mwaka mmoja kamili tangu tarehe ambazo zilikuwa zimepangwa kufanyika kwa michezo ya Olimpiki yam waka huu 2020.

Thomas Bach, Rais wa Kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC anasema, “hii leo tumeweka tarehe za michezo ya Olimpiki yam waka huu 2020 mjini Tokyo kuwa zitafanyika mwaka ujao wa 2021. Kwa michezo ya Olimpiki, kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 8 Agosti na michezo ya Paralimpiki kuanziatarehe 24 mwezi Agosti hadi tarehe 5 mwezi Septemba.”

Uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia maazimio matatu makuu na kulingana na kanuni zilizowekwa na Bodi ya Utendaji ya IOC (EB) mnamo tarehe 17 Machi 2020 na kudhibitishwa katika mkutano wake uliofanyika jumatatu wiki hii. Maazimio haya yaliunga mkono na na shirikisho la kimataifa la michezo ya Olimpiki ya majira ya kiangazi na kamat zote za kitaifa za za Olimpiki (NOCs).

Bwana Bach, anaongeza kusema, “tulichagua tarehe hizi kufuata kanuni zetu, ambazo tulizianzisha tarehe 17 Machi, na hii ni, kwanza kabisa, kulinda afya ya mtu yeyote anayehusika katika Michezo ya Olimpiki na kutoa mchango wetu katika kuvidhibiti virusi - ukweli ambao imekubaliwa, miongoni mwa wengine wengi, pia na mkutano mkuu wa G20 hivi karibuni. Na tulilazimika kuangalia katika kalenda ya michezo ya kimataifa ili kudumisha umoja wa Michezo ya Olimpiki. Pamoja na sababu hizi, sasa tunaweza kutarajia kuwa na Michezo hii msimu ujao wa kiangazi, ambao ni kipindi ambacho pia kinaweza kusimamiwa na wadau wetu wajapan na marafiki kwa sababu mara zote walisema tarehe katika msimu wa joto wa mwaka 2021.”

Taarifa ya awali ya OIC imesema kuwa wanamichezo wote ambao tayari walikuwa wamefuzu na tayari wamepangiwa kushiriki katika michezo ya Olimpiki yam waka 2020 watasalia kama walivyo bila kubadilishwa. 

Rais wa OIC amesema hata hivyo kwamba mabadiliko haya ni changamoto kubwa kwani watahitaji kubadilisha vitu vingi ikiwemo namna ya kushughulika na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa tayari vimejipanga kupeperusha matangazo ya michezo hii. Ametaja pia kuwa changamoto kubwa itakuwa kuhusu wadhamini ambao nao walikuwa tayari kwa ajili ya mwaka huu.

Wakati huo huo mwenge wa Olimpiki ambao tayari ulikuwa umewasili nchini Japan tangu tarehe 20 ya mwezi huu wa Machi, utaendelea kuwaka kwa mwaka mzima hadi michuano hii itakapochezwa mwakani. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter