Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa msaada wa barakoa 250,000 kwa mji wa New York

Umoja wa Mataifa wakabidhi barakoa 250,000 za kitabibu kwa Meya wa New York
UN Photo/Eskinder Debebe)
Umoja wa Mataifa wakabidhi barakoa 250,000 za kitabibu kwa Meya wa New York

UN yatoa msaada wa barakoa 250,000 kwa mji wa New York

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ametangaza kwamba pamopja na balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Kelly Craft wametoa msaada wa barakoa 250,000 zilizo kwenye maduka ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwa serikali ya Marekani.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake Guterres amesema barakoa hizo ambazo ni za ziada baada ya kutimiza mahitaji ya Umoja wa Mataifa zitagawiwa kwa wahudumu wa afya mjini New York ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa ujasiri, kujitoa kimasomaso na bila kuchoka kukabiliana na kusambaa kwa mlipuko wa virusi vya Corona COVID-19 katika mabara yote yam ji huo, akitumai kwamba zitasaidia japo kwa kiasi kidogo kuokoa maisha.

Umoja wa Mataifa wamkabidhi Meya wa New York Barakoa za kitabibu 250,000
UN Photo/Eskinder Debebe)
Umoja wa Mataifa wamkabidhi Meya wa New York Barakoa za kitabibu 250,000

 

Katibu Mkuu amesema “tunaongea kwa sauti moja kuonyesha mshikamano wetu kwa mji huu mzuri na watu wake. Kwetu sisi New York sio tu ni nyumbani kwetu au makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Ni mji mashuhuri wa kimataifa ambao kupitia huo dunia inawasiliana , kujadiliana, kufanya biashara na kushamiri. Kwa niaba ya jumuiya ya Umoja wa Mataifa na wanadiplomasia tunatumai mchango huu mdogo utaleta mabadiliko.”

Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa kwa sasa wanashirikiana na ofisi ya meya wa New York kuhakikisha kwamba vifaa hivyo vya msaada vinafikishwa kwa njia bira na salama kwenye vituo vya afya kwenye maeneo yote ya mji wa New York.