Shirika la kazi duniani, ILO limesema kuwa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, limeweka hadharani udhaifu wa masoko ya ajira duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Rider amesema kampuni kuanzia ndogo hadi kubwa tayari zimesitisha operesheni zao, nyingine zimepunguza saa za kazi na hata kupunguza wafanyakazi, “nyingine ziko hatarini kusambaratika kwa kuwa maduka yamefungwa, safari za ndege na miadi ya hoteli inafutwa na biashara sasa zinafanyika kutokea majumbani.”
Hata hivyo amesema kundi la kwanza la waajiriwa lililo hatarini ni makarani wa mauzo, wahudumu hotelini na migahawani, wapishi, wapagazi na wasafishaji.
Mtu 1 kati ya 5 anastahili mafao ya ukosefu ajira
“Katika dunia ambayo ni mtu 1 tu kati ya 5 ambao wana sifa za kupata mafao ya kukosa ajira, suala la kupunguza wafanyakazi linaleta janga kubwa kwa mamilioni ya famlia,” amesema Bwana Ryder akifafanua kuwa likizo ya kuuguza si kwa kila mtu anayemhudumia mgonjwa au kila mfanyakazi anayewasilisha mizigo au huduma majumbani na maofisini, “ambao sote tunawategemea hivi sasa na ambao wanakuwa katika shinikizo la kuendelea kufanya kazi hata kama ni wagonjwa.”
Mkurugenzi Mkuu huyo wa ILO amesema na katika nchi zinazoendelea, vibarua na wafanyabiashara wasio rasmi nao pia wanaweza kuwa kwenye shinikizo litokanalo na mahitaji ya familia zao.
Kutokana na hali hiyo, Bwana Ryder anasema kuwa, “sote tutapata matatizo kwa sababu siyo tu itaongeza kuenea kwa virusi bali pia katika kipindi cha muda mrefu itaongeza na kuendeleza mzunguko wa umaskini na ukosefu wa usawa.”
Ili kuondokana na udhaifu huo uliojitokea, Mkurugenzi Mkuu huyo wa ILO anasema kuwa kuna fursa ya kuokoa mamilioni ya ajira na kampuni, “iwapo serikali zitachukua hatua thabiti kuhakikisha biashara zinaendelea, zizuie watu kupunguzwa kazi na kulinda wafanyakazi waio hatarini.”
Uamuzi wa leo utamuathiri kila mtu
Anaongeza kuwa uamuzi unaochukuliwa hii leo ni dhahiri utakuwa na athari kwa afya ya jamii na uchumi kwa miaka mingi ijayo.
“Sera zisizo za kawaida za fedha ni muhimu ili kuzuia mporomoko wa sasa usiwe mdororo wa muda mrefu wa uchumi. Lazima tuhakikishe watu wana fedha za kutosha mifukoni mwao ili wakidhi mahitaji yao muhimu na mengineyo,” amesema Ryder akiongeza kuwa hatua hiyo inamaanisha kuhakikisha kampuni ambazo ni vyanzo vya mapato kwa wafanyakazi zinaweza kuendelea kuwa na fedha ata wakati mdororo na zinakuwa tayari kuendelea pindi hali inapokuwa nzuri.
Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa ILO amesema kadri serikali zinavyojaribu kupunguza kasi ya maambukizi, “tunahitaji hatua maalum za kulinda mamilioni ya wahudumu wa afya, wengi wao wakiwa ni wanawake ambao wanaweka maisha yao hatarini kila siku kutuhudumia. Madereva wa lori, mabaharia ambao kila siku wanasafirisha na kuwasilisha shehena za matibabu na vifaa vingine muhimu, hawa nao wanapaswa kulindwa.”
Amesisitiza kuwa kufanyia kazi nyumbani, kunatoa fursa kwa mwajiriwa kuendelea kufanya kazi na mwajiri kuendelea na shughuli zake wakati wa majanga, “lakini waajiriwa wanapswa kuwa na uwezo wa majadiliano kuhusu ufanyaji kazi kutokea nyumbani ili waweke mizania ya wajibu mwingine kama vile kulea watoto, kuhudumia wagonjwa na wazee na bila shaka wao wenyewe.”
ILO inakadiria kuwa takribani wafanyakazi milioni 25 watakosa ajira, idadi ambayo shirika hilo linasema itaweza kuwa kubwa zaidi.