Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo kutokana na COVID-19 duniani sasa 21,031, OCHA yahofia kwenye mizozo na majanga

Watoto waliotawanywa wakila chakula katika pango walimokuwa wamejihifadhi katika kijiji cha Taltouna nchini Syria
© UNICEF/Ali Haj Sulei
Watoto waliotawanywa wakila chakula katika pango walimokuwa wamejihifadhi katika kijiji cha Taltouna nchini Syria

Vifo kutokana na COVID-19 duniani sasa 21,031, OCHA yahofia kwenye mizozo na majanga

Amani na Usalama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA leo imezungumzia hofu yake jinsi majanga na mizozo inavyoendelea kuwa kikwazo katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 huko Syria, Libya na Afghanistan huku ikipongeza hatua zilizochukuliwa na Sudan katika kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo.

Msemaji wa OCHA, Jens Laerke akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi ameanza na Syria akisema kuwa “Umoja wa Mataifa una wasiwasi kuwa COVID-19 itaathiri mamilioni ya watu nchini Syria hususan watu 900,000 ambao bado wametapakaa kaskazini-magharibi mwa taifa hilo baada ya kukimbia makwao.”

Amesema mlundikano wa watu hao unafanya wawe hatarini zaidi na kwamba maandalizi ya kukabiliana na magonjwa nchini Syria bado ni madogo kwa kuwa, “ni nusu tu ya hospitali na vituo vya msingi vya afya nchini humo vilikuwa vinafanya kazi mwishoni mwa mwaka jana na maelfu ya wataalamu wa afya wamekimbia nchi hiyo.”

Huko Libya, Bwana Laerke amesema hofu kubwa ni kwamba mlipuko wa COVID-19  unaweza kuzidia uwezo operesheni za usaidizi wa binadamu ambazo tayari zimetindikiwa.

Amesema ingawa Umoja wa Mataifa unasaidia mamlaka za Libya katika kujiandaa kukabiliana na COVID-19, bado fedha zaidi zinahitajika haraka kutekeleza mipango ya kitaifa na umoja huo kwa sekta ya afya.

Na zaidi ya yote amesema kuwa wana  hofu kubwa kwa sababu uhasama umendelea kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli na viunga vyake licha ya ombi la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa kwa mapigano na uhasama ili kupatia kipaumbele masuala ya kibinadamu na kukabili COVID-19.

Kwa upande wa Sudan, OCHA imenukuu taarifa ya Wizara ya Afya nchini humo ya kutangaza bajeti ya dola milioni 76 za kukabiliana na COVID-19 nchini humo huku mipango mingine ya kimajimbo dhidi ya ugonjwa huo ikiendelea kupangwa.

“Mathalani huko Darfur magharibi, mamlaa zimefunga mpaka na Chad tangu tarehe 17 mwezi huu wa Machi, na marufuku ya safari za mabasi baina ya majimbo nchini Sudan imeanza kutekeleza tangu jana tarehe 26 mwezi Machi huku misafara ya shehena za kibinadamu, biashara na vifaa vya ufundi ikiendelea,” amesema Bwana Laerke.

Msemaji huyo wa OCHA ameongeza kuwa viwanja vya ndege vya kimataifa na kitaifa vimefungwa hadi tarehe 23 mwezi ujao wa Aprili huku lakini ndege zenye shehena za kibinadamu na biashara zikiruhusiwa kutua.

Nchini Iraq ambako hadi tarehe 26 mwezi huu wa Machi imethibitisha wagonjwa 382 wa COVID-19 na vifo 36, tayari wahudumu wa kibinadamu wameandaa hatua usaidizi kwenye kambi za wakimbizi na tayari mwongozo wa kukabiliana na ugonjwa huo umesambazwa kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo nchini Afghanistan, OCHA inasema kuwa hofu kubwa ni maeneo ya kuvuka mipaka, kuepusha mikusanyiko na marufuku ya kutembea.

Hofu hiyo kwa muijbu wa Laerke ni kubwa kwa kuzingatia kuwa, virusi vya Corona vimethibitishwa katika majimbo 12 ya Hirat, Samangan, Balkh, Daikundi, Farah, Kapisa, Badghis, Logar, Zabul, Kandahar, Ghazni na Kabul.

Halikadhalika amesema idadi kubwa ya watu nchini Afghanistan waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo waliwahi kusafiri nje ya nchi.

Bwana Laerke amegeukia Iran akisema kuwa inaendelea kupigwa na majanga matatu ya kidharura ambayo ni kuongezeka kwa wagonjwa wa virusi vya Corona, mafuriko na baa la nzige.

“Mvua kubwa zimeathiri majimbo 11, watu 11 wamefariki dunia hadi sasa, baa la nzige linatishia maeneo ya kilimo kwenye majimbo 6. Lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa yanachukua hatua za usaidizi nchini Iran,” ametamatisha msemaji huyo wa OCHA.

Hadi leo tarehe 27 Machi 2020, COVID-19 imethibitishwa katika mataifa 199 ambapo kuna jumla ya wagonjwa 465,915 na kati yao 21,031 wamefariki dunia.