25 Machi 2020

Ni rahisi sana kuhisi kuzidiwa uwezo na kila kitu pindi unaposikia kuhusu ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19. Ni wazi kuwa watoto wanapata shaka na shuku hasa wanapoona taarifa kwenye runinga au kusikia kutoka kwa watu. Je utazungumza nao vipi? Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limekupatia vidokezo vifuatavyo ili uweze kuibua mjadala na watoto na kuzungumza nao.

1. Uliza maswali ya kufikirisha na sikiliza

Anza kwa kumwalika mtoto wako azungumze juu ya virusi vya Corona. Tafiti kiwango cha uelewa wao na fuata mwongozo wao. Iwapo bado ni wadogo na hawajasikia juu ya mlipuko, huenda hautahitaji kuibua suala hilo - chukua nafasi hiyo kuwakumbusha juu ya tabia nzuri za usafi bila kuibua hofu mpya.
Hakikisha uko katika mazingira salama na umruhusu mtoto wako azungumze kwa uhuru. Michoro, hadithi na shughuli zingine zinaweza kusaidia kufungua mjadala.

Muhimu zaidi, usipunguze au usiepuke shaka na shuku zao. Hakikisha unatambua hisia zao na kuwahakikishia kuwa ni kawaida kuhofia mambo hayo. Onesha kuwa unasiliza kwa kuwa makin, na hakikisha wanaelewa kuwa wanaweza kuzungumza nawe na walimu wao wakati wowote ule wanaopenda.

2. Kuwa mwaminifu; eleza ukweli kwa njia ya kirafiki na watoto

Watoto wana haki ya kupata habari za ukweli juu ya kile kinachotokea katika ulimwengu, lakini watu wazima pia wana jukumu la kuwalinda salama dhidi ya kukanganyikiwa. Tumia lugha inayoendana na umri wao, angalia wanavyopokea taarifa hizo na kuwa mwangalifu na kiwango chao cha wasiwasi.

Katu usikisie iwapo huwezi kujibu maswali yao. Tumia hali hiyo kama fursa ya kutafiti majibu pamoja. Wavuti ya mashirika ya kimataifa kama shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na lile la afya WHO ni vyanzo vikubwa vya habari. Wafafanulie ya kwamba baadhi ya taarifa kwenye mtandao si sahihi na kwamba ni bora kuwaamini wataalam.

3. Waoneshe jinsi ya kujilinda na marafiki wao

Njia moja bora zaidi ya kuwalinda watoto dhidi ya virusi vya Corona na magonjwa mengine ni kuhamasisha unawaji wa  mikono. Hili halipaswi kuwa gumzo la kutia hofu. Imbeni au chezeni dansi ili somo hili liwe la kuvutia.
 
Pia unaweza kuonesha watoto jinsi ya kujifunika na kiwiko cha mkono pindi unapokohoa au kupiga chafya, na uwaeleze kuwa ni bora kutokuwa karibu na watu wenye dalili za ugonjwa wa virusi vya Corona na waombe wakueleze pindi tu watakapoanza kuhisi kama wana homa, kikohozi au shida ya kupumua.

4.Wapatie hakikisho

Tunapoona picha nyingi za kutisha kwenye runinga au simu ya rununu, wakati mwingine unaweza kuhisi kana kwamba shida iko karibu nasi. Watoto wanaweza kushindwa kutofautisha kati ya picha kwenye televisheni na hali yao ya kibinafsi, na wanaweza kuamini kuwa wako katika hatari kubwa. Unaweza kusaidia watoto wako kukabiliana na mfadhaiko kwa kuwapatia fursa ya kucheza na kupumzika, inapowezekana. Weka mara kwa mara ratiba na ratiba iwezekanavyo, haswa kabla ya kulala, au kusaidia kuandaa mpya katika mazingira mapya.
 
Iwapo kuna mlipuko kwenye eneo lenu, kumbusha watoto wako ya kwamba wanaweza wasipate ugonjwa, na kwamba watu wengi wanaoambukizwa COVID-19 hawaugui sana na zaidi ya yote watu wazima wanahaha kuhakikisha familia zinakuwa salama. Na iwapo mtoto wako hajisikii vizuri, mweleze kwamba wanapaswa kusalia nyumbani au hospitali kwa sababu ni salama zaidi kwao na kwa rafiki zao. Wahakikishie kwamba unafahamu ni vigumu na pengine wakati mwingine inachosha au inatisha, lakini kufuata kanuni kutasaidia kumweka kila mtu salama.

5. Angalia iwao wanakabiliwa au wanaeneza unyanyapaa

Mlipuko wa COVID-19 umeleta ripoti nyingi za ubaguzi wa rangi kote ulimwenguni, kwa hivyo ni muhimu kuangalia kuwa watoto wako hawanyanyapaliwi na wala hawasababishi uonevu.

Fafanua kwamba virusi vya Corona havina uhusiano wowote na muonekano wa mtu, anakotoka au lugha anayozungumza. Ikiwa wamepachikwa majina majina au wameonewa shuleni, wanapaswa kujisikia huru kumweleza mtu mzima ambaye wanamwamini.  Kumbusha watoto wako kuwa kila mtu ana haki ya kuwa salama shuleni. Uonevu shuleni ni kosa na kla mmoja anapaswa kuchukua hatua kueneza ukarimu na kusaidiana.

 

6. Tafuta wasaidizi

Ni muhimu kwa watoto kufahamu kuwa watu wanasaidiana kwa matendo ya fadhili na ukarimu.

Wapatie watoto simulizi za wahudmu wa afya, wanasaynsi na vijana, miongoni mwa mifano michache, ambao wanafanya kazi kuzuia mlipuko na kuweka jamii salama. Inaweza kuwa faraja kubwa kufahamu kwamba watu wenye huruma wanachukua hatua.
 

7. Jitunze

Utaweza kusaidia watoto wako vizuri zaidi iwapo nawe unakabiliana vyema na hali iliyopo. Watoto wataangalia ni vipi unachukua hatua kutokana na habari zinazotangazwa. Hii inasaidia wao kutambua iwapo unahimili hali ilivyo na unatulia. Ikiwa unahisi hofu au kukasirika, jipe wakati mwenyewe na saka  ushauri kutoka kwa familia nyingine, marafiki na watu wanaoaminika katika jamii yako. Tafuta wakati wa kufanya vitu  ambavyo vinakusaidia kupumzika na kupona.

8. Hitimisha mazungumzo kwa uangalifu

Ni muhimu kutambua kuwa huwaachi watoto katika hali ya mkanganyiko. Mazungumzo yanapokaribia kufikia tamati, jaribu kupima kiwango cha wasiwasi kwa kutazama lugha ya mwili wao, ukizingatia kama wanatumia sauti yao ya kawaida na pima kauli zao kwa kusikiliza pumzi zao.

Wakumbushe watoto wako kuwa wanaweza kuwa na mazungumzo mengine magumu na wewe wakati wowote. Wakumbushe kwamba unajali, unasikiliza na kwamba unapatikana kila wanapohisi kuwa na wasiwasi.

 
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud