Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen sitisheni uhasama mjikite na COVID-19:Guterres

Mvulana akiwa amesimama mbele ya magofu huko Saada, Yemen.
WFP/Fares Khoailed
Mvulana akiwa amesimama mbele ya magofu huko Saada, Yemen.

Yemen sitisheni uhasama mjikite na COVID-19:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa pande kinzani katika mzozo wa Yemen kusitisha uhasama mara moja na kujikita katika majadiliano ya suluhu ya kisiasa huku wakifanya kila wawezalo kukabiliana na virusi vya Corona, COVID-19.

Katika taarifa iliyotolewa kupitia msemaji wake Jumanne jioni Antonio Guterres amesema zaidi ya miaka mitano ya machafuko imesambaratisha maisha ya mamilioni ya raia wa Yemen.

Na machafuko yanayoendelea hivi sasa katika maeneo ya Al Jawf na Ma’rib yanatishia kuongeza madhila ya kibinadamu kwa watu hao.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote kushirikiana na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo ili kufikia lengo la kusitisha mapigano nchi nzima , kupiga hatua katika mchakato wa kiuchumi na masuala ya kibinadamu ambayo yatawapunguzia madhila rai ana kuwajengea ujasiri, pia ametaka kuanza tena kwa mchakato jumuishi wa kisiasa unatakaoongozwa na Wayemeni wenyewe.

Guterres amesisitiza kwamba suluhu ya kisiasa ndio suluhu pekee kuelekea muafaka wa kina na endelevu kwa mzozo wa Yemen.