Wafanyakazi wenye ulemavu CCBRT Tanzania wapatiwa mafunzo ya dhidi ya COVID-19

23 Machi 2020

Nchini Tanzania mafunzo kuhusu virusi vya Corona na jinsi ya kukabiliana navyo ambayo yanatolewa kwa watendaji wenye ulemavu katika hospitali ya CCBRT yemekuwa na manufaa makubwa wakati huu ambapo tayari taifa hilo la Afrika Mashariki limethibitisha kuwa na wagonjwa wa virusi hivyo. Ni kwa vipi basi? Tuungane na Hilda Phoya mwanafunzi anayefanya mafunzo kwa vitendo katika kituo cha habari za Umoja wa Mataifa, UNIC jijini Dar es salaam ambaye amevinjari katika hospitali hiyo.

Nimefika katika hospitali ya CCBRT iliyopo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam ili kufahamu uelewa wa watendaji wenye ulemavu katika kukabiliana na virusi vya Corona.

Baada ya kutumia viuavisumisho ili kutakatisha mikono yangu nakutana na Abdalla Majule, mfanyakazi  CCBRT ambaye amenieleza..“Nimejifunza vizuri zaidi tofauti na mwanzo nilikuwa naona kwenye vyombo vya habari na kusikia. Leo nimepata kitu kikubwa, kwa sababu tumefundishwa vizuri jinsi gani ya kujikinga. Kama una virusi vya Corona ni vyema wewe ukavaa barakoa kuliko yule ambaye hana Corona, vinginevyo wale wanaohudumia wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya Corona wao ndio wanaweza kuvaa barakoa.”

Naye Jestina Mdoe ambaye ni kiziwi akizungumza kupitia mtafsiri wa lugha, Suzan, ameshukuru mafunzo waliyopatiwa ya kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya Corona lakini amezungumzia suala la kuwapatia viziwa habari akisema, “Mara nyingine tunapata usiku kwenye televisheni mbalimbali,  na baadhi ya sisi tunaotumia lugha ya alama, lakini wakati mwingine tunapata vikwazo, kwa sababu watu wanaozungumza na wanaosikia wao wanaelewa, lakini sisi viziwi tunatumia lugha ya alama. Ni lazima tuweze kuona na  kama mkalimani yupo kwenye televisheni sauti au picha ni ndogo, kwa hiyo mimi na matatizo ya macho inawezekana kuangalia sielewi na picha yenyewe siwezi kuona na kuielewa vizuri. Kwa hiyo naomba sana kuwasisitiza viziwi waalikwe na lugha ya alama itumike kuwapatiwa mafunzo na Mungu awabariki.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

COVID-19 Tanzania: Wafanyabiashara ndogo ndogo wazungumza

Nchini Tanzania  maambukizi ya virusi vya Corona au COVID-19 yameendelea ambapo hii leo wagonjwa wapya wawili wote wakazi wa Dar es salaam wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo baaada ya mmoja kuingia nchini kutoka safari ya Denmark, Uswisi na Ufaransa huku mwingine akiwa amerejea kutoka Afrika Kusini.

COVID-19 Tanzania : Wagonjwa wafikia 3, Vyuo Vikuu vyafungwa, mgonjwa wa kwanza azungumza.

Nchini Tanzania idadi ya wagonjwa wa Corona au COVID-19 imefikia 3 baada ya wagonjwa wapya wawili kuthibitishwa hii leo wakiwa ni raia wa Marekani na Ujerumani.