Tuachane na ukataji miti ili kuufanya mwaka huu wa 2020 kuwa ‘mwaka mkuu wa asili’-Guterres

21 Machi 2020

Leo dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa ya misitu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatoa wito kuwa mwaka huu wa 2020 ambao umeelezwa kuwa ‘mwaka mkuu wa asili’ uwe mwaka ambao ulimwengu uipe kisogo tabia ya ukataji miti na uteketezaji misitu.

Siku ya kimataifa ya mwaka huu imejikita katika kuonesha uhusiano kati ya misitu na baionwai kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2019 ambayo ilitahadharisha kuhusu kuongezeka kwa kasi ya kutoweka kwa aina mbalimbali za viumbe na kasi ya ajabu ya namna baionwai inavyopungua.

Misitu na machaguo yetu yasiyo endelevu

Katibu Mkuu Guterres ameeleza kuwa misitu, na mazingira ya ulimwengu kwa ujumla, yanamomonyolewa na njia zetu zisizo endelevu tunapotumia maliasili, hali ambayo inaongeza kasi ya upotezaji wa baionwai na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.

Kwa kuzingatia jukumu kubwa ambalo misitu inachangia katika kuhifadhi uhai duniani na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, Bwana Guterres ametahadharisha kuhusu uharibifu unaofanywa na hali ya ukame katika sehemu nyingi za ulimwengu, akitoa mfano wa moto wa misitu kuanzia kule Canada na Siberia hadi California na Australia.

 

Juu ya hayo, ukataji miti unaendelea kutokea, kwa sababu ya kilimo kikubwa: ingawa kiwango cha mwaka cha ukataji miti kimepungua kwa miaka 25 iliyopita, maeneo makubwa ya misitu yanaendelea kupotea.

"Tunatakiwa kuchukua hatua haraka kurekebisha hili. Kulinda misitu ni sehemu ya suluhisho.” Amesema Bwana Guterres akizisii serikali, biashara na asas iza kiraia kuchukua hatua za haraka kusitisha ukataji mitin a kurejesha misitu ili vizazi vijavyo viweze kufurahia mstakabali ulio wa kijani na wenye afya.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud