Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwenye vita watu milioni 100 wako hatarini kwa COVID-19:OCHA

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaelezea wasiwasi wao kuhusu watu milioni 100 wanoishi maeneo ya vita wanaohitaji msaada.
UNOCHA/Iason Athanasiadis
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaelezea wasiwasi wao kuhusu watu milioni 100 wanoishi maeneo ya vita wanaohitaji msaada.

Kwenye vita watu milioni 100 wako hatarini kwa COVID-19:OCHA

Afya

Wakati virusi vya Corona , COVID-19 vikiendelea kusambaa kote duniani Umoja wa Mataifa unatiwa hofu kuhusu athari kwa watu milioni 100 wanaoishi katika maeneo ya vita na dharura nyingine ambao wanategemea misaada ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masula ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHADunia ni lazima iendelee kuwasaidia wasiojiweza ikiwemo kupitia msaada wa kibinadamu unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa  na mpango wa msaada kwa wakimbizi.”

Jens Laerke ambaye ni msemaji wa OCHA ameongeza kuwa kwa ujumla mashirika ya misaada yanahofia kuhusu upungufu wa mifumo ya ufuatiliaji katika baadhi ya nchi ambako maelfu ya watu wasiojiweza wanaishi. “Nchi hizi huenda hazina miundombinu ya kukabiliana na athari kubwa za mlipuko huo wa COVID-19.”

Suala linguine amesema ni mrundikano wa makambi ya wakimbizi wa ndani katika sehemu zenye majanga ya kibinadamu hali ambayo inaleta hatari kubwa ya COVID-19. OCHA inasema watu wengi wanaishi katika mazingira magumu na hawana kabisa au wanazo kidogo sana huduma za msingi za usafi na afya.

 

“Wakati virusi vinafika katika sehemu hizi athari zake zinaweza kuwa mbaya sana. Na mlipuko mpya wa COVID-19 utaongeza gharama kubwa kwa maisha ya wat una jamii hasa ambazo kwa sasa zinakabiliwa na matatizo mengine ya kiafaya kama surau na homa ya manjano ambayo hayapatiwi uzito mkubwa.”

UN yaomba ufadhili wa fedha wiki ijayo

Zaidi ya changamoto zote hizo athari katika mnyororo wa usambazaji inamaanisha kwamba lishe ya kukabiliana na utapiamlo inayozalishwa katika nchi moja inaweza isifike katika nchi nyingine ambako inahitajika.

Kwa sasa mashirika ya misaada ya kibinadamu yanajiandaa kusitisha program za mlo mashuleni. OCHA inasema pia maji na usafi vinaweza visitosheleze au kutopatikana kabisa. “Vituo vya usambazaji wa misaada ambako watu wengi hukusanyika kwa ajili ya chakula au misaada mingine huenda ikakatazwa na suluhu mbadala zitahitajika.”

Bwana Laerke amesema katika hali hii lengo la jumuiya ya misaada ni kuendelea kutoa msaada muhimu wa kuokoa maisha huku ikichukua hatua Madhubuti kuepuka zjanga kubwa linaloweza kusababishwa na COVID-19 kwa watu hawa wenye uhitaji mkubwa.

Kwa sasa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatathimini wapi operesheni za kibinadamu zinapatwa na dosari na kuweza kusaka suluhu.

Pia Umoja wa Mataifa unalifanyia kazi suala la mpango thabiti wa masuala ya kibinadamu ambao unatarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo.

“Ili kuikomesha COVID-19, inabidi kuikomesha kila mahali.Endapo hatutokomesha maambukizi duniani kote , virusi vinaweza kurejea kwenye nchi ambazo zilidhani ziko salama” limesisitiza shirika la OCHA na kuongeza kwamba kuendelea na hatua za kibinadamu kukabiliana na janga hili ni kitendo cha mshikamano wa kimataifa na pia ni ishara ya ubinadamu.