Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji ya wanawake yapatiwe kipaumbele wakati wa COVID-19: UN Women

Manusura wa ukatili wa kingono akiwa Monrovia, Liberia.
UN Photo/Staton Winter
Manusura wa ukatili wa kingono akiwa Monrovia, Liberia.

Mahitaji ya wanawake yapatiwe kipaumbele wakati wa COVID-19: UN Women

Afya

Wakati janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 likiendelea kutikisa duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women linashirikiana na wadau wake kuhakikisha kuwa madhara ya ugonjwa huo katika jinsia yanaepukika.

UN Women inatolea mfano karantini zinapowekwa ina maana wanawake na wasichana wanapaswa kusalia ndani ya familia zao na iwapo wamekuwa wanakabiliwa na ukatili wa kingono, inakuwa ni fursa kwa wale wakatili wao kuendelea kufanya vitendo hivyo.

Sarah E Hendriks ambaye ni Mkurugenzi wa Sera, Mipango katika UN Women amesema kuwa ripoti kutoka baadhi ya jamii zinazokumbwa na ukatili zimedhihirisha kuwa COVID-19 inachochea mienendo kama hiyo kule kwenye karantini.

Halikadhalika amegusia suala la uchumi akisema kuwa, ugonjwa wa Corona utaathiri wanawake zaidi hasa wale wanaofanya kazi za ujiro mdogo, na kwenye sekta zisizo rasmi na wasio na uhakika wa kipato.

Amesema kuwa zuio la kutembea linaweza kuathiri zaidi uwezo wa wanawake kujipatia kipato na kukidhi mahitaji muhimu ya familia yao kama ambavyo ugonjwa wa Ebola ulivyoleta madhara kwenye vipato vya wanawake.

Bi. Hendriks amesema ni kwa mantiki hiyo wanashirikiana na wadau wao kuanzia ngazi ya serikali hadi kikanda kuhakikisha kuna mikakati ya kusaidia mahitaji ya wanawake wakati huu COVID-19 inaendelea kusambaa.

Mathalani kusaidia kukusanya data zenye mnyumbuliko wa kijinsia ili mahitaji ya wanawake yasiwekwe kando, kujikita katika miradi ambayo inajenga mnepo wa wanawake kwa janga la sasa na majanga yajayo, ili kuhakikisha wana rasilimali wanazohitaji wao wenyewe na familia zao.

Afisa huyo wa UN Women ametolea mfano China ambako amesema wanajikita katika kusaidia wanawake kujikwamua baada ya ugonjwa wa Corona kwa kusaidia biashara ndogo na za kati zinazomilikiwa na wanawake na pia walisaidia kampeni za kusongesha uongozi wa wanawake katika harakati za kukabiliana na mlipuko wa Corona na waliweza kufikia zaidi ya watu milioni 32.

Amekumbusha kuwa ni lazima jamii itambue kuwa, “kadri maeneo mengi yanavyofungwa hususan shule, fursa ya wanawake kupata muda wa ziada na kutoka kujipatia kipato inapungua na hivyo ni lazima kuwekwa kwa mikakati mbadala kuweza kuwasaidia ili waweze kujinusuru.”