Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 Tanzania : Wagonjwa wafikia 3, Vyuo Vikuu vyafungwa, mgonjwa wa kwanza azungumza.

Shughuli za ununuzi kwenye duka jijini Dar es Salaam, Tanzania wakati huu ambapo kumeripotiwa kutangazwa kwa visa vya corona nchini humo.
UN News/ Stella Vuzo
Shughuli za ununuzi kwenye duka jijini Dar es Salaam, Tanzania wakati huu ambapo kumeripotiwa kutangazwa kwa visa vya corona nchini humo.

COVID-19 Tanzania : Wagonjwa wafikia 3, Vyuo Vikuu vyafungwa, mgonjwa wa kwanza azungumza.

Afya

Nchini Tanzania idadi ya wagonjwa wa Corona au COVID-19 imefikia 3 baada ya wagonjwa wapya wawili kuthibitishwa hii leo wakiwa ni raia wa Marekani na Ujerumani. 

Taarifa za kuthitbishwa kwa wagonjwa hao wapya zimetolewa leo mjini Arusha nchini Tanzania na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisema kuwa,  "sampuli ya kwanza ni ya raia wa Marekani mwenye umri wa miaka. 61 ambaye ni mkazi wa Dar es salaam. Mgonjwa huyu sasa hiv iamewekwa mahala maalum kwa ajili ya taratibu nyingine za matibabu ikiwemo kufuatilia watu waliokuwa karibu naye.  Sampuli ya pili ambayo imefanyiwa vipimo na kuthitishwa kuwepo kwa virusi vya Corona ilipokelewa kutoka Zanzibar ambayo ilipokelewa kutoka Zanzibar ni ya mwanaume mwenye umri wa miaka 24 raia wa Ujerumani.”

Waziri Ummy akatoa wito kwa wananchi akiwataka , "kutokuwa na hofu kwa kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa ugonjwa huu unadhibitiwa nchini kwetu.”

Na hatua zaidi za kudhibiti kusambaa kwa COVID-19 zikatangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es salaam ambaye amesema kuwa, "sasa leo tunaendelea kuongeza vyuo vya elimu ya kati na Vyuo Vikuu vyote nchini navyo pia tunasitisha kuendelea na masomo. Tunatambua Vyuo Vikuu wanafunzi wengi wako likizo na sasa tunawataka wasirudi kwenye vyuo vyao, na wale wachache waliokuwa wamebaki kwa mitihani nao pia waondoke mara moja  kwenye vyuo hivyo ili kuondoa  misongamano kwenye maeneo hayo. Bado shughuli za maduka na masoko zitaendelea. Na natamka hili kwa sababu tumeanza kuona mkanganyiko mkubwa kwenye maeneo ya masoko na maduka.  Huduma za usafirishaji nazo zitaendelea, wasafirishaji waendelee kuwaelimisha abiria, wale wakibaki kwenye viti magari yaende.”

Naye mgonjwa wa kwanza wa Corona Tanzania, Isabella Mwampamba akazungumza kwa njia ya simu na wana habari kutoka eneo alilotengewa kuhusu hali yake ya sasa.

(Sauti ya Isabella Mwampamba)