Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inaendelea kuangalia usalama wa wakimbizi katika mpaka wa Sudan na Chad

Leo nchini Chad kuna takriban watu 657,000 waliofurushwa makwao asilimia 51 ni wanawake na wasichana.
OCHA/Naomi Frerotte
Leo nchini Chad kuna takriban watu 657,000 waliofurushwa makwao asilimia 51 ni wanawake na wasichana.

UNHCR inaendelea kuangalia usalama wa wakimbizi katika mpaka wa Sudan na Chad

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linategemea siku za hivi karibuni kufanya awamu ya pili ya uhamishaji wa wakimbizi wa Sudan waliokimbilia nchini Chad.

“Awamu ya kwanza ya uhamisho ilitekelezwa kati ya tarehe 6 na 13 ya mwezi huu wa Machi ambapo watu 4,559 sawa na familia 1,145 wamehamishwa kutoka katika mpaka wa Chad na Sudan na kuwasogeza ndani katika kambi ya Koichaguine Moura.” Imefafanua taarifa ya UNHCR.

Hitaji la kuwahamisha wakimbizi hao lilikuja baada ya mnamo tarehe 27 mwezi wa pili mwaka huu wa 2020, tathimini kuonesha kuwa kutokana na hali inayoleta wasiwasi mpakani, kulikuwa na haja ya kuwahamisha kwa haraka watu ambao wanawanahitaji haraka ulinzi hususani wale waliokuwa katika eneo la Ardebe.

UNHCR inasema kuwa inafanya maandalizi ya miundombinu katika kambi ya Koichaguine Moura ili kuwapokea wakimbizi wengine.

Aidha UNHCR imearifu kuwa hali nchini Sudan bado inasalia kuwa tete na isiyotabirika lakini watu wanaokimbia wamepungua ingawa pia shirika hilo la kuhudumia wakimbizi linaendelea kufuatilia kinachoendelea mpakani.