Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa nina miaka 11 najihisi nina miaka 100: mtoto Naamat

Nchini Syria watoto wakibebwa kwenye lori wakati familia zikikimbia machafuko jimbo la Idlib.
© UNICEF/Forat Abdoullah
Nchini Syria watoto wakibebwa kwenye lori wakati familia zikikimbia machafuko jimbo la Idlib.

Ingawa nina miaka 11 najihisi nina miaka 100: mtoto Naamat

Amani na Usalama

Wakati vita vya Syria vikiwa vimetinga miaka tisa sasa maelfu ya watoto maisha yao yanaendelea kuwa njiapanda wengi wakiwa wamepoteza wazazi na kila kitu na wengine kulazimika kukua kuliko umri wao.

Hiyo ni sauti ya Naamat akisema nina umri wa miaka 11 lakini najihisi kama nina miaka 100, ni mkimbizi kutoka Homs Syria ambaye sasa anaishi Jordan, vita vya miaka tisa vimemfanya abebe majukumu yanayozidi umri wake.

Kila uchao mama yake anapokwenda kazini inambidi ashike majukumu yake, ikiwemo kumvalisha  na kumwenya maziwa mdogo wake mdogo “Mdogo wangu haniiti dada, ananiita mama”

Kisha anaandaa kifungua kinywa kwa ajili ya wadogo zake wengine wawili wavulana kabla ya kufanya usafi na kutayarisha mabegi yao tayari kwenda kupanda basi la shule. Anasema si kupenda kwake,“Ni kwa sababu ya hali inayotukabili, inanibidi niwasaidie wazazi wangu na kaka zangu. Hawana mtu mwingine mimi ndio mkubwa.”

Baba wa Naamat ni mgonjwa na hawezi kufanya kazi yoyote, na mama yake Fatima anafanyakazi ya kusafisha nyumba za watu kutwa nzima. Fatima anasema, “Wakati mwingine nahisi kama ni mkubwa kuliko mimi na ananipa ushauri”

Licha ya majukumu yote hayo na umri mdogo juhudi zake zimemfanya Naamat ashamiri nyumbani na shuleni,“Nimepoteza sehemu ya utoto wangu lakini sehemu nyingine kama elimu, kusoma na kujenga mustakabali wangu haijapotea, sintokata tamaa."

Naamat mwenye ndoto za kuwa rubani siku moja anasema hatoacha changamoto anazopitia sasa zizime ndoto zake za kuwa na maisha mazuri na mustkabali bora hapo baadaye.