Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Sudan Kusini kwa kuunda Baraza la Mawaziri- Guterres

Hatua ya kuundwa Baraza la Mawaziri inafuatia kuapishwa kwa viongozi wakuu akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar na kuapishwa tarehe 22 Februari mwaka 2020 mjini Juba.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Hatua ya kuundwa Baraza la Mawaziri inafuatia kuapishwa kwa viongozi wakuu akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar na kuapishwa tarehe 22 Februari mwaka 2020 mjini Juba.

Heko Sudan Kusini kwa kuunda Baraza la Mawaziri- Guterres

Amani na Usalama

Hatua ya serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa nchini Sudan Kusini kuunda Baraza la Mawaziri imepongezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Taarifa ya msemaji wake iliyotolewa jijini New York, Marekani Ijumaa usiku imemnukuu akipongeza utashi wa pande zote kulegeza misimamo y ao na kufanikisha hatua hiyo muhimu. “Nasihi vyama vya kisiasa nchini Sudan Kusini na viongozi wao kufanya juhudi za ziada ili kufikisha lengo la kuwa na asilimia 35 ya uwakilishi wa viongozi wanawake kwenye mchakato wote wa amani,” amesema Katibu Mkuu Guterres. Ametoa wito pia kwa viongozi kwenye taifa hilo change zaidi duniani kupatia kipaumbele utekelezaji wa taratibu za mpito kwenye suala la usalama na pia waongeze juhudi zao katika kushughulikia mapigano ya kikabila, ukwepaji sheria na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu. Halikadhalika amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa katika kusaidia pande husika kutekeleza mkataba mpya wa amani uliotiwa saini mwezi Septemba mwaka 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia, kwa ushirikiano na mamlaka ya maendeleo ya mataifa, IGAD pamoja na Muungano wa Afrika, AU. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Baraza hilo la Mawaziri linamjumuisha Bi. Angelina Teny, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Bi. Teny ni mke wa Riek Machar, kiongozi wa zamani wa upinzani ambaye wiki iliyopita alikubaliana na Rais Salva Kiir kuunda serikali ya mpito.