Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na wadau wasaka dola bilioni 1.3 kwa ajili ya wakimbizi Sudan Kusini

Mgao wa chakula huko Peri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini  ya miaka mitano. (Picha  5 Februari 2019)
WFP/Gabriela Vivacqua
Mgao wa chakula huko Peri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)

UNHCR na wadau wasaka dola bilioni 1.3 kwa ajili ya wakimbizi Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na washirika wake wanasaka dola bilioni 1.3 mwaka huu ili kushughulikia mahitaji makubwa ya kibinadamu kwa wakimbizi wanaofungasha virago na kukimbia vita vya miaka saba nchini Sudan Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa shirika hilo la UNHCR Babar Baloch amesema wanakaribisha kuundwa kwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini , lakini bado kuna changamoto nyingi zilizosalia katika kusaka suluhu kwa mamilioni ya raia wa nchi hiyo ambao wanalazimika kutawanywa na machafuko. na kuongeza kuwa,“Idadi kubwa kabisa ya wakimbizi Afrika ni kutoka Sudan Kusini. Takribani watu milioni 2.2 wamelazimika kukimbia makwao na wengi wao asilimia 83 ni wanawake na Watoto. Na wengine milioni 2 zaidi wametawanywa ndani ya nchi.”

UNHCR inasema watu wameendelea kutawanywa mwaka 2019 ambapo zaidi ya wakimbizi 74,000 kutoka Sudan Kusini walisaka hifadhi Uganda, Sudan, Kenya, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Baloch amesisitiza kwamba,“Fedha za ufadhili zinahitajika haraka ili kutoa msaada wa kuokoa Maisha ambao unajumuisha kuwahudumia watoto wakimbizi 65,000 ambao wako peke yao au wametenganishwa,fursa ya kupata maji salama ya kunywa  na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kingono na kijinsia. “

Ameongeza kuwa pia pengo linaendelea katika elimu ya wakimbizi na kuna haja ya kuanzisha shughuli zitakazowaruhusu wakimbizi kupata ujuzi ili kuwawezesha wajitegemee pamoja na familia zao.

UNHCR imehimiza kwamba msaada unahitajika kwa nchi zote tano zinazohifadhi wakimbizi hawa kutoka Sudan Kusini kwani zimeendelea kuacha milango yao wazi kuwapokea na miongoni mwa nchi hizo Ethiopia, Kenya na Uganda zimethibitisha ukarimu  wa aina yake kwa kuwakumbatia wakimbizi na kuwa na sera ya wakimbizi kuishi nje ya makambi na kuwajumuisha katika huduma za jamii.

Tangu mwaka 2017 zaidi ya wakimbizi 270,000 wamerejea Sudan Kusini kwa hiyari yao lakini wengi wao ambao bado wako nje ya nchi wanasubiri kuona endapo amani itatudumu.