Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 mzozo wa Syria amani bado kitendawili:Guterres

Nour, 16, anasimama katika kitongoji chake kilichosambaratishwa na vita katika eneo la Karm Al-zaitoun katika mji wa Homs, Syria.
©UNICEF/Abdulaziz Al-Droubi
Nour, 16, anasimama katika kitongoji chake kilichosambaratishwa na vita katika eneo la Karm Al-zaitoun katika mji wa Homs, Syria.

Miaka 10 mzozo wa Syria amani bado kitendawili:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mzozo wa Syria ukiingia mwaka wa 10 bado amani inaonekana kuwa ni ndoto.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani Guterres amesema,“mzozo huo wa kikatili umesababisha gharama kubwa na janga la kibinadamu lisiloelezeka. Mamilioni ya raia wanaendelea kukabiliwa na hatari za ulinzi, zaidi ya nusu ya watu wamelazimika kukimbia nyumba zao huku mamilioni wengine wanaoishi katika mazingira hatari kama wakimbizi na watu wengine milioni 11 wanaendelea kuhitaji msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha. “

Katibu Mkuu ameongeza kwamba dunia imeona miaka tisa ya ukatili mbaya sana, pamoja na uhalifu wa vita.

Miaka tisa ya unyanyasaji wa haki za binadamu kwa kiwango kikubwa wa kimfumo, kutozingatia kanuni za kimataifa kwa hali mpya ya  ukatili na mateso. Pia amesema “maelfu ya watu hawajulikani waliko, wametoweka, wamefungwa, wananyanyaswa na kuteswa. Idadi isiyojulikana wameuawa na kujeruhiwa. Lazima ihakikishwe hakuna ukwepaji wa sheria kwa  uhalifu mbaya kama huo.”

Usaidizi wa kibinadamu

Hata hivyo mkuu huyo wa Umoja wa Matraifa amesema kwa wakati wote wa vita mifumo ya kibinadamu imetumia kila njia iliyowezekana kuwafikishia msaada wale walio na uhitaji kuanzia kuidondosha kwa njia ya anga hadi usafiri mbalimbali ikiwemo kuvuka mipaka. Mwaka 2019 Umoja wa Mataifa na washirika wake waliwafikia watu zaidi ya milioni 6 kila mwezi katika nchi nzima Syria.

Mwezi Januari mwaka huu msaada wa chakula kwa watu takribani milioni 1.4 ulifikishwa kwa njia za kupitia mipakani pekee  vikiwemo vifaa tiba vya kuwasaidia watu wapatao nusu milioni na vifaa vingine ambavyo si chakula kwa zaidi ya watu 230,000.

Hatua za kuwapunguzia madhila raia wa Syria

Guterres amesema hatua za kuwapunguzia madhila mamilioni ya raia wa Syria zinajulikana na zinapaswa kutekelezwa “Mosi ni makubaliano ya tarehe 5 Machi ya kutrejesha utulivu na kusitisha machafuko Idleb yaliyofanywa baiana ya Urusi na Uturuki  ni lazima yawe muongozo wa kuelekea muafaka wa kudumu wa kukomesha uhasama ambao utafungua njia ya ukomeshaji mapigano wa kutumu kote nchini Syria. Na pili pande zote zinapaswa kurejea kwenye mchakato wa kisiasa unaoswezeshwa na Umoja wa Mataifa chini ya azimio namba 2254 (2015) ambalo linasalia kuwa ndio njia pekee ya kumaliza mzozo na kutoa suluhu ya kudumu kwa watu wa Syria.”

 Katibu Mkuu ametoa wito akisema, “ujumbe watu leo uko bayana hatuwezi kuruhusu mwaka wa 10 wa mzozo ukasababisha zahma ileile, ukiukwaji uleule wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu na vitendo vilevile vya kikatili”.