Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa kulinda mamilioni ya wasichana dhidi ya ndoa ya watoto kuendelea kwa miaka minne

Amaboua anahudhuria vipindi kuhusu athari za ndoa za ututoni kwenye jamii yake nchini Chad.
UNFPA/Ollivier Girard Michel
Amaboua anahudhuria vipindi kuhusu athari za ndoa za ututoni kwenye jamii yake nchini Chad.

Mpango wa kulinda mamilioni ya wasichana dhidi ya ndoa ya watoto kuendelea kwa miaka minne

Haki za binadamu

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF, na la idadi ya watu UNFP yametangaza leo mjini New York Marekani kuwa, mkakati wa nchi nyingi kutokomeza ndoa za utotoni na kusaidia kulinda haki za mamilioni ya wasichana utafanyika tena kwa kipindi cha miaka minne zaidi.

Kufikia mwaka 2023, programu ya pamoja ya UNFPA na UNICEF kutokomeza ndoa za utotoni itawakuwa imewafikia zaidi ya mabinti milioni 14 katika nchi 12 barani Afrika, Mashariki ya kati na Asia Kusini. Programu hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa mnamo mwaka 2016, pia inahusisha familia, waelimishaji, watoa huduma, serikali, viongozi wa dini na kimila kama sehemu ya juhudi za ulimwengu kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema, “tangu kuzinduliwa, mpango wa dunia umeokoa mamilioni ya wasichana dhidi ya ndoa zisizohitajika. Pia tunatakiwa tusisahau wasichana milioni 12 ambao bado wanaolewa kila mwaka na kusababisha madhara ambayo hayawezi kurekebishika kwa mstakabali wa maisha yao, afya na ustawi wao. Miaka minne ijayo ya mpango huu inatoa fursa mpya kuendeleza kasi yetu tulipofikia na kutokomeza milele matendo haya ya kusikitisha.”

Awamu ya pili ya programu iliyozinduliwa katika msingi na mazingira ya kampeni ya Kizazi cha Usawa na pia wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya Mkataba wa Beijing na Jukwaa la Hatua itaendelea kuangazia mikakati inayotambulika, ikiwemo kuongeza nafasi ya wasichana kupata elimu na huduma za kiafya, kuendeleza ujuzi, kuwaelimisha wazazi na jamii kuhusu hatari za ndoa za utotoni na pia kukuzausawa wa kijinsia, kujenga ushirikiano kwa kutoa msaada wa kiuchumi kwa familia na kuimarisha na kutekeleza sheria ambazo zinaeleza kuwa miaka 18 ndio umri wa chini wa ndoa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Natalia Kanem amesema, “ikiwa mabinti watakuwa wanaendelea kuolewa wakiwa bado wadogo, hatuwezi kufikia usawa wa kijinsia ambao vijana wadogo wanauhitaji. Wasichana wanatakiwa kuwa na nguvu ya kufanya machaguo yao wenyewe, yaani ni wakati gani nan ani wa kuoana naye, kuhusu kuendelea na elimu, na kuhusu iwapo wapate watoto na lini.Mpango huu umepanga kuwawezesha wasichana kutekeleza haki zao, kutimiza uwezo wao na kuleta mabadiliko katika jamii zao.”

Tangu programu hiyo ilipozinduliwa mwaka 2019, zaidi ya wasichana wadogo 7.7 na wana jamii milioni 4.2 wamefikiwa na taarifa, ujuzi na huduma. Programu hii pia imezisaidia serikali kuendeleza na kutekeleza mikakati ya kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni.

Duniani kote, inakadiriwa kuwa wasichana na wanawake milioni 650 walioko hai hii leo, waliolewa wakiwa watoto, ambapo takribani nusu yao wanaishi katika nchi ambazo hivi sasa zinasaidiwa na mpango huo wa Umoja wa Mataifa kutokomeza ndoa za utotoni.

 

TAGS: UNFPA, UNICEF, Ndoa za utotoni