Utalinda vipi watoto dhidi ya Corona?

Utalinda vipi watoto dhidi ya Corona?
Mashirika hayo lile la afya, WHO na lile la kuhudumia watoto, UNICEF na mdao wao shirikisho la msalaba na hilal nyekundu duniani, IFRC wamesema hayo kupitia taarifa yao iliyotolewa Jumanne kwenye miji ya Geneva, Uswisi na New York, Marekani.
“Mwongozo huo unatoa masuala muhimu na vigezo vya kuzingatia ili maeneo ya shule yawe salama. Pia unatoa ushauri kwa mamlaka za kitaifa na manispaa kuhusu jinsi ya kutekeleza mipango ya dharura kwa ajili ya maeneo ya shule,” imesema taarifa hiyo.
Je mwongozo una nini?
Mathalani pindi shule zinapofungwa, mwongozo unapendekeza hatua za kuchukua ili kupunguza hatua hiyo isiwe na madhara kwa uwezo wa mtoto kujifunza na ustawi wake.
“Hii inamaanisha kuwa na mipango thabiti ya mtoto kuweza kuendelea kusoma hata kama yupo nyumbani kama vile elimu mtandao, na elimu kupitia matangazo ya radio na wakati huo huo mtoto apate huduma muhimu. Mipango hiyo ijumuishe pia hatua salama za kuhakikisha pindi shule zifunguliwapo zinaendelea kuwa salama kwa mtoto,” umefafanua mwongozo huo wa UNICEF, WHO na IFRC.

Na iwapo shule zinasalia zimefunguliwa, mashirika hayo yamependekeza kuwa ni lazima kuhakikisha watoto na familia zao wanaendelea kulindwa, wanapata taarifa na hivyo mwongozo unasema kwamba, “ watoto wapatiwe taarifa ya jinsi ya kujilinda, wafundshwe jinsi ya kunawa mikono vizuri sambamba na kupatiwa vifaa vya kujisafi. Kuwepo pia na mfumo mzuri wa kupitisha hewa.”
Mashirika hayo yameongeza pia, “majengo ya shule yawe yanafanyiwa usafi kwa kutumia dawa za kuua vijidudu.”
Mwongozo ni hata kwa wasio na COVID-19
Mashirika hayo yamesema ingawa mwongozo ni kwa nchi ambazo zimeshathibitisha kuwa na wagonjwa wa COVID-19, bado ni muhimu katika mazingira mengine.
Yamekumbusha kuwa, miongozo ya shule salama iliyotumika huko Guinea, Liberia na Sierra Leone wakati wa mlipuko wa Ebola mwaka 2014 hadi 2016, ilisaidia kuzuia maambukizi ya virusi hivyo shuleni.
Mambo mengine ya kuzingatia, mashirika yametaka afya ya mtoto ifuatiliwe na iwapo anaugua abakie nyumbani, kuhamasisha watoto kuuliza maswali na kuelezea shaka na shuku zao, kukohoa na kupiga chafya kufanyikie kwenye kitambaa au kwenye kona ya kiwiko na kuepusha kugusa uso, macho, mdomo na pua.