Sasa virusi vya Corona vina dalili ya kuenea duniani kote- WHO

11 Machi 2020

Hatimaye ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 umetangazwa kuwa sasa una dalili ya kuenea duniani kote, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza na wanahabari mjini Geneva, Uswisi hii leo.

Dkt. Tedros amesema hatua ya kutangaza kuwa virusi vya Corona vimeenea duniani ni kwa kuzingatia kuktwa hivi sasa kuna zaidi ya wagonjwa 118,000 katika mataifa 114 ambapo tayari watu 4,291 wamefariki dunia.

“Maelfu wengine wako taabani hospitali wakihaha kuokoa maisha yao. Katika siku na wiki zijazo, tunatarajia kuwa idadi ya wagonjwa itaongezeka, sambamba na idadi ya vifo na idadi ya nchi yenye wagonjwa halikadhalika. WHO imekuwa ikitathmini mlipuko na tumekuwa na hofu kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huu na vile vile ukosefu wa uchukuaji  hatua,” amesema Dkt. Tedros.

Amesema ni kwa kuzingatia hilo wametathmni na kubaini kuwa COVID-19 sasa inaweza kuwa imeenea duniani kote.

Dkt. Tedros amekumbusha kuwa neno  kwamba una mwelekeo umeenea duniani kote au kwa kiingereza, pandemic  si neno la kutumia kwa urahisi tu au bila umakini. “Ni neno ambalo iwapo litatumika vibaya linaweza kusababisha hofu isiyotakiwa au watu kukubali bila sababu ya kwamba tumeshindwa kupigana vita dhidi ya ugonjwa vimekwisha na hivyo kusababisha machungu na vifo.”

Hata hivyo amekumbusha kuwa kwa kutangaza kuwa ugonjwa huo umeenea dunia nzima, “hakubadili tathmini ya WHO ya tishio litokanalo na virusi hivyo. Haibadilishi kile ambacho WHO inafanya na haibadilishi kile ambacho nchi zinapaswa kufanya.”

Ni mara ya kwanza virusi vya Corona kusambaa dunia nzima

Kwa mujibu wa Dkt. Tedros, hii ni mara ya kwanza kwa virusi hivi ya Corona kusambaa dunia nzima akisema kuwa, “katu hatujawahi kuona kusambaa kwa ugonjwa utokanao na virusi vya Corona. Hili ni janga la kwanza la kusababishwa na virusi vya Corona. Na wakati huo huo katu hatujawahi kuona ugonjwa ulioenea duniani kote ambao unaweza kudhibitiwa .”

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa WHO imekuwa ikichukua hatua tangu ilipoarifiwa kisa cha kwanza na hivyo wanatoa wito kwa nchi kuchukua hatua za dharura na za haraka akisema kuwa, “tumegonga kengele kwa sauti kubwa na inayosikika.”

Katika wiki mbili zilizopita, idadi ya wagonjwa wa COVID-19 nje ya China imeongeza mara 13, huku idadi ya nchi nazo zenye wagonjwa zikiongezeka mara 3.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter