Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa lazima yafundishe watoto wa kiasili na wale wa jamii za wachache kwa lugha yao wenyewe - mtaalam wa UN

Lugha mbalimbali
UNESCO
Lugha mbalimbali

Mataifa lazima yafundishe watoto wa kiasili na wale wa jamii za wachache kwa lugha yao wenyewe - mtaalam wa UN

Utamaduni na Elimu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya makabila madogo, kupitia ripoti yake aliyoiwasilisha hii leo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi amesema ni lazima watoto wanaotoka  jamii za wachache, wafundishwe kwa lugha yao inapowezekana ili kufikia lengo la ujumuishwaji na elimu bora pamoja na kuheshimu haki za binadamu za watoto wote.

Akiwasilisha ripoti hiyo mtaalamu huyo Fernand de Varennes amesema kuwa elimu katika lugha mama ya makabila hayo ya watu wachache, ikiunganishwa na ufundishaji bora wa elimu rasmi, ni gharama nafuu na inapunguza idadi ya wanaoacha masomo, na inasababisha matokeo bora ya masomo hususan kwa wasichana.

Ameongeza kuwa inaboresha viwango vya kujua kusoma na kuandika kwa lugha zote yaani lugha mama na lugha iliyo rasmi au inayozungumzwa na wengi na hivyo kuongeza ushiriki mkubwa wa familia na jamii.

Katika ripoti yake, mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa tafiti nyingi zinakubali kuwa matumizi mazuri ya lugha hizo za wachache au zisizozungumzwa na wengi, katika elimu, zinaweza kuongeza ushirikikishwaji, mawasiliano na kuamini kati ya wanajamii wa jamii ndogo na mamlaka za mataifa husika.

Ameenda mbali akifafanua kuwa watoto kutoka katika jamii za asili au za wachache watakuwa na matokeo mazuri ya masomo na watasalia shuleni kwa muda mrefu wanapofundishwa kwa kutumia lugha ambayo wameizoea zaidi, mara nyingi ile lugha yao.

Bwana de Varennes amesema hali hiyo inapotokea, hususani wanapobaki zaidi shuleni, si tu watapata msingi imara na uelewa wa kusoma na kuandika kwa lugha yao, pia wataweza kuimudu vizuri lugha rasmi au lugha inayotumiwa na wengi.

Ameonya kuwa kutokutumia lugha ya wachache kama lugha ya kufundishia, mahali ambapo inawezekana, inamaanisha kutoa elimu ambayo haina thamani au matokeo sawa.

Kwa hivyo Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa ametroa wito wa kuandaliwa maelekezo yanayotekelezeka yanayotoa mwongozo kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu za jamii za wachache na matumizi ya lugha zao katika nyanja ya elimu.