Chonde chonde virusi vya Corona visilete rabsha kwenye elimu - UNESCO

10 Machi 2020

Idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya Corona ikiongezeka duniani sambamba na watu waliofariki dunia, Umoja wa Mataifa umetaka hatua zichukuliwe ili kuepusha janga hilo kusambaratisha elimu wakati huu ambapo hatua zinazochukuliwa kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo ni pamoja na kufunga shule na vyuo vikuu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kwa kutambua uwezekano huo leo liliitisha mkutano wa maafisa waandamizi wa elimu kutoka nchi mbalimbali duniani, mkutano uliofanyikwa kwa njia ya video ukiratibiwa kutoka makao makuu ya shirika hilo mjini Paris, Ufaransa.

Kikao hicho cha dharura kimejumusha wawakilishi kutoka mataifa 72 wakiwemo mawaziri 27 wa elimu na wawakilishi waandamizi 37.

Takwimu za UNESCO zinaonyesha kuwa janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19 limeathiri takribani wanafunzi milioni 363 duniani kote kuanzia wale wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.

"Mwanafunzi 1 kati ya 5 duniani kote hivi sasa haendi shule kwa sababu ya virusi vya Corona na mwingine 1 kati ya 4 analazimika kutokwenda chuo cha elimu ya juu. Nchi 15 zimeagiza shule zote kufungwa nchini mwao na 14 zimechukua hatua za kufunga shule kulingana na eneo ilipo, kuanzia Asia, Ulaya, Mashariki ya Kati hadi Amerika ya Kaskazini," imesema UNESCO.

Ni kwa mantiki hiyo, Mkrugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay akizungumza kwenye mkutano huo amesema kuwa, "tunaingia eneo ambalo hatujalizoea na tunashirikiana nan chi kusaka suluhu kupitia teknolojia za juu sana, za kati au hata kusiko na teknolojia kuhakikisha kuwa masomo yanaendelea. Kadri nchi zinavyojiandaa kuchukua hatua, ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kubadilishana mbinu fanisi na kusaidia wanafunzi, walimu na familia zao."

Ameongeza kuwa UNESCO inaongeza usaidizi wake kuhakikisha janga la Coroa linachochea ubunifu na ujumuishi badala ya kuongeza pengo katika kujifunza.

Tayari UNESCO imeunda kikosi kazi cha dharura dhidi ya COVID-19 kusaidia hatua za kitaifa na sera bora, kikimulika nchi zilizo hatarini zaidi.

Shirika hilo linalenga kuhamasisha sekta binafsi na wadau kama vile Microsoft tayari wamejuuishwa kwenye kikosi kazi hicho.

Pamoja na kuunda kikosi kazi hicho, UNESCO imeweka kwenye mtandao jukwaa la kusaidia wanafunzi, wazazi na walimu pamoja na shule katika kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa njia ya mtandao.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter