Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shida za kijamii na kisiasa zafurusha raia 4,000 wa Nicaragua kila mwezi- UNHCR

Waandamanaji mjini Managua wakidai kukomeshwa kwa ghasia nchini Nicaragua
Artículo 66
Waandamanaji mjini Managua wakidai kukomeshwa kwa ghasia nchini Nicaragua

Shida za kijamii na kisiasa zafurusha raia 4,000 wa Nicaragua kila mwezi- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani miaka miwili tangu Nicaragua itukumbukie kwenye mzozo wa kisiasa na kijamii, zaidi ya watu 100,000 wamekimbia nchi hiyo na kusaka hifadhi nje ya nchi ili kukwepa mateso na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Shabia Mantoo amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo ya kwamba hata baada ya ghasia za awali kupungua mwezi Aprili mwaka 2018, “wanafunzi, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wakulima wameendelea kukimbia taifa hilo kwa kiwango cha wastani wa watu 4,000 kila mwezi. Suluhu ya mzozo ikionekana kuwa bado ni ndoto, UNHCR inatarajia idadi hiyo kuongezeka.”

Idadi kubwa ya wakimbizi hao kutoka taifa hilo la Amerika ya Kati, kwa mujibu wa UNHCR, wanakimbilia kwanza Costa Rica ambayo sasa inahifadhi theluthi mbili ya wakimbizi wote wa Nicaragua na wasaka hifadhi, ambao ni 77,000.

Wengine zaidi ya 8,000 wamekimbilia Panama, na wengine 9,000 Ulaya huku Mexico ikihifadhi wakimbizi 3,600. Wakimbizi wengine 5,100 wamesaka hifadhi kwenye mataifa mengine na kufanya jumla ya wanicaragua wakimbizi na wasaka hifadhi duniani kote kufikia 103,600.

UNHCR inasema kuwa tangu mwezi Oktoba mwaka jana wa 2019, Costa Rica kwa usaidizi wa shirika hilo, imekuwa na mchanganuoa wa kimakini kwa wasaka hifadhi wanaothibitishwa kukimbia mateso Nicaragua kwa kupunguza wao kutambuliwa wakimbizi, na hivyo kuwapatia ulinzi.