Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wafunga safari hatari kusaka maisha bora Amerika

Ndugu wawili Romeu na Kulutwe kutoka Angola wakiwa na familia zao wakivuka mto Tuquesa kuelekea Bajo Chiquito ambacho ni kijiji cha kwanza nchini Panama katika mpaka wa Colombia
© UNICEF/William Urdaneta
Ndugu wawili Romeu na Kulutwe kutoka Angola wakiwa na familia zao wakivuka mto Tuquesa kuelekea Bajo Chiquito ambacho ni kijiji cha kwanza nchini Panama katika mpaka wa Colombia

Watoto wafunga safari hatari kusaka maisha bora Amerika

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema idadi ya watoto waliovuka pori la Darien linalotenganisha Colombia na Amerika ya Kati mwaka 2019 imeongezeka zaidi ya mara saba ikilinganishwa na mwaka 2018. 

UNICEF inasema kuwa watoto waliovuka eneo hilo mwaka 2019 imefikia takribani 4,000  ikilinganishwa na watoto 522 mwaka  wa 2018 na watoto hao ni kutoka zaidi ya mataifa 50 yakiwemo India, Somalia, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Bangladesh.

Takribani asilimia 50 ya watoto hao wana umri wa chini ya miaka 6 na takwimu zinatoka katika ofisi ya uhamiaji ya kitaifa.

Video ya UNICEF inaonesha watoto hao wakikatisha pori na kuvuka mito na mabonde ambapo shirika hilo linaonya kuwa hatari wanazokumbana nazo watoto hao wahamiaji na familia zao katika safari hizo ni kubwa mno.

Hatari hizo ni pamoja na kukosa maji safi na salama, kukumbwa na hatari za kiasili, wanyama, uporaji, ukatili na kutumikishwa.

Watoto hao wahamiaji mwisho wa safari  yao ni Panama ambapo UNICEF inasema pindi wanapowasili wanapokewa katika kituo cha makazi cha mapokezi huko La Peñita kwenye jimbo la Darien, moja ya majimbo yaliyo nyuma zaidi kimaendeleo nchini humo.

Kutoka hapo watoto wanasafirishwa na mamlaka za uhamiaji hadi jimbo la Chiriqui kwenye mpaka na Costa Rica huku wengi wao wakitarajiwa kuendelea na safari hadi Marekani au Canada.

UNICEF inasema inachofanya sasa kwa kushirikiana na wadau ni kusaidia juhudi za Panama za kulinda haki za watoto hao walio kwenye msafara na pindi wanapokuwa kwenye mpito Panama.

Hatua hizo ni pamoja na kujenga uwezo wa mashinani na kitaifa katika kusambaza huduma za kibinadamu, kuchunguza hali ya lishe, ujauzito na huduma za ujazi kwa wahamiaji wanaowasili.

Halikadhalika kuweka mifumo  ya maji ambapo kila siku zaidi ya lita 30,000 za maji zinapelekwa kwa wahamiaji na wenyeji wao pamoja na shuleni na taasisi za serikali.

Tatu ni kusaidia huduma za kujisafi na kuweka maeneo salama ya watoto ambako watoto wahamiaji an wenyeji wanaweza kucheza na kupatiwa huduma za kuwasaidia makuzi yao na pia akina mama wanaweza kunyonyesha watoto wao kwa usalama zaidi.

Kwa kuwa idadi ya watoto wahamiaji wanaotarajiwa kuvuka pori la Darien itaendelea kuongezeka, UNICEF inasema itaendelea kuwepo na kutoa huduma hizo muhimu hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2020.