Waliopona Ebola huko Beni watoa shukrani zao

9 Machi 2020

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, baadhi ya wanawake waliopona ugonjwa wa Ebola wametoa shukrani zao kwa mamlaka kwa kuwa hivi sasa wanaweza kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

Miongoni mwa manusura hao wa mlipuko huu wa 10 wa Ebola nchini humo ni Kahindo Fazila Mayamoto, mwenye  umri wa miaka 23, mkazi wa Beni jimbo la Kivu Kaskazini na mama wa watoto 4 anasema, "kwa kweli mimi nilikuwa na manung’uniko sana kwa sababu tulipoteza watu wanane kwa sababu ya Ebola. Mimi na watoto wangu watatu na mume wangu tumepona, kwa kweli inanitia moyo sana na nishakuwa na nguvu, na kwa kweli kwa sababu bado tunawasikiliza wale waliotutunza na bado wanatusaidia na  wanatuletea chakula. Kwa kweli nishajisikia huru, Niko vyema na nishaelewa kuwa Ebola ni ugonjwa na kumbe waliopona wanaweza kuelimisha wengine.”

Kahindo akaenda mbali zaidi akisema, "na tunakuwa na ujasiri wa kuelimisha wanawake wenzetu ili waone kuwa ilikuwa ni ugonjwa wa kweli na tushapona na tushakuwa na nguvu na sasa tunafanya kazi vizuri. Tunashirikiana na hata wale ambao hawakuugua. Kwa kweli nashukuru sana kwa kweli wanawake wote nawahamasisha tushirikiane.”

Mgonjwa mwingine wa Ebola aliyepona ni Masika Semida Muhasu, mwenye umri wa miaka 54 na mkazi pia wa Beni ambaye anatambuliwa kuwa mgonjwa wa mwisho wa Ebola nchini DRC, "nafurahi sana kabisa huu ugonjwa mkali  umemaliza watu wengi hapa Beni, mimi najisikia huru kabisa,  mimi ni wa mwisho na ugonjwa huu  ufunge virago kabisa, naomba Mungu sana. Mungu atufunike ili huu ugonjwa usirudi tena niwe mimi wa mwisho.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter