CSW64 ni fursa ya kuchagiza kasi ya kufikia usawa wa kijinsia:UN

9 Machi 2020

Kikao cha 64 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW64 kimeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani , ingawa hakitofanyika kwa wiki mbili kama ilivyo ada. 

Kikao hicho ambacho hufanyika kila mwaka kikiwaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia kuanzia Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia, wanawake wa mashinani na wanaharakati wa masuala ya wanawake, safari hii kinafanyika kwa siku moja tu na kisha kuahirishwa hadi itakapotangazwa tena. Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuchukua tahadhari dhidi ya mmlipuko wa virisi vya Corona au COVID19 unaoendelea kusambaa duniani.

Akifundua rasmi kikao hicho cha siku moja leo mjini New York Marekani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema,“Kamisheni hii ni fursa ya kuchagiza zaidi kasi ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake ambayo inaongezeka kote duniani. Ninawataka kutumia kikao hiki kujikita na nini kinachotuunganisha na kusistiza ahadi ya azimio la Beijing na jukwaa la kuchukua hatua kwa kikamilifu, utekelezaji wake kamili, madhubuti na wenye kasi.”

Katika kikao hiki cha siku moja wajumbe ambao ni wawakilishi wa kudumu wa nchi wanachana kwenye Umoja wa Mataifa wnatoa tarifa mbalimbali za nchi zao kuhusu hali ya wanawake na kupitisha azimio la kisiasa llakini pia wanachukua hatua dhidi ya miswada ya maazimio mengine yaliyowasilishwa. Akihimiza umuhimu wa kuifanya karne hii kuwa ni kizazi cha usawa wa wanawake Guterres amesema, “hebu na tutume ujumbe uliobayana kwa dunia kwamba haki za wanawake ni haki za binadamu na kwamba usawa wa kijinsia ni kitovu cha malengo yote ya maendeleo endelevu.”

Mwaka 2020 ni mwaka wa wanawake na wasichana

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake Phumzile MIambo-Ngcuka akizungumza kwenye kikao hicho cha 64 amesema mwaka huu wa 2020 ni mwaka mahsusi kwa ajili ya usawa wa kijinsia kwani ni miaka 25 tangu kupitisha azimio la Beijing na jukwaa lka kuchukua hatua kuhusu haki za wanawake.

Ameongeza kuwa leo hii cha msingi ni kusonga mbele ambapo azimio la kisiasa limepitishwa linalosisitiza jukwaa la Beijing la kuchukua hatua na pia kupitishwa kwa program yam waka ujao ya CSW.

Mbali ya kuadhimisha miaka 25 ya azimio la Beijing Bi. Ngukca amesema “Mwaka huu tunaadhimisha miaka 20 ya utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama namba 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama lakini pia ni miaka 10 ya UN Women na kuanza kwa muongo wa kuchukua hatua kuhusu SDGs.”

Ameongeza kuwa maadhimisho yote haya ni kusherehekea utekelezaji wa ahadi ya kimataifa lakini amesisitiza kwamba wanawake kote duniani wanapoteza uvumilivu kutokana na hatua za kuboresha maisha yao ambazo haziridhishi.

“Wanashuhudia juhudi zilizopigwa zikirudishwa nyuma, wanaona kwamba kasi ya mabadiliko haiendi kamainavyotakiwa, wasichana hawataki kuyapitia yale waliyoyapitia wazee wao na wazee wamechoka kusibiri”

Mafanikio yaliyopatikana

Mkuu huyo wa UN Women amesema pamoja na kuenfdelea kuwepo kwa changamoto lakini kuna hatua chanya zilizopatikana ikiwa ni pamoja nan chi 131 kuchukua hatua za kisheria na kufanyia marekebbisho maeneo muhimu yahusuyo haki za wanawake, nchi nyingi zaidi zimeanzisha, kuimarisha au kutekeleza sheria dhidi ya ukatili kwa wanawake, wasichana wengi zaidi wanahudhuria shule sasa kuliko awali, serikali nyingi na wasichana wenyewe wanafanya kila wawezalo kukomesha ndoa za utotoni na hatua kubwa imepigwa katika vita dhidi ya ukeketaji au FGM.

Kazi nyingi ujira kidogo

Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio yote hayo bado mamilioni ya wanawake na wasichana wanataabika na kujikuta kwenye hofu ya kuachwa nyuma kwani pengo la usawa wa kiuchumi halijabadilika katika miaka 20 iliyopita.

“Hakujakuwa na mabadiliko yoyote makubwa katika ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake katika miaka 20 iliyopita isipokuwa Amerika ya Kusini, wanawake milioni 740 wamekwama katika uchumi wa sekta isiyo rasmi, wakipata ujira mdogo na kuwa na usalama mdogo au kuukosa kabisa.” Hili ameongeza kuwa ni kichocheo kikubwa cha kuwaacha wanawake kwenye mzunguko wa umasikini. Akitoa mfano amesema wasichana wanaolea familia wako asilimia 25 zaidi ya uwezekano wa kuishi katika ufukara kuliko wanaume na kupata athari za muda mrefu katika maisha yao.

Ili kubadili hali hii Bi. Ngukca ametoa wito akisistiza mshikamano wa kila mmoja kwamba “Kwa pamoja tunaweza kufanya mabadiliko tunayoyataka, kwa pamoja ni jamii yenye usawa tunayoitaka.”

Kusuasua kwa hatua za usawa wa kijinsia kunatuathiri sote:Bande

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Tijjan Mohammed-Bande amesema “mabadiliko yamekuwa yajijikongoja kwa wanawake wengi na wasichana kote duniani na kwa minajili hiyo jamii nzima imekuwa ikiathirika, na hakuna nchi hata moja inayoweza kusema imetimiza usawa wa kijinsia.

Na kwa mantiki hiyo amehimiza “Ni lazima tusongeshe mbele mchakato katika ngazi zote na tukianza muongo wa kuchukua hatua katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu kwa mara ya kwanza tunatathimini mchakato wa jukwaa la Beijing kwa minajili ya ajenda ya 2030.”

Bwana Bande amesisistiza kwamba tusifanye makosa kwani “Ni muhimu kwamba kujumuisha suala la usawa wa kijinsia katika kazi zetu zote endapo tunataka kufikia lengo lolote la SDG. Hatuwezi kuitenga asilimia 50 ya watu wote, ni wajibu wa kila mtu kutekeleza ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma.”

Ametoa wito wa kufanya kazi pamoja kuelekea kutokomeza mifumo yote ya ubaguzi ambayo ambayo haina faida yoyote katika karne hii ikiwemo ubaguzi wa rangi, jinsia na ukatili wa aina zote ukiwemo ukatili wa kijinsia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter