Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naibu Katibu Mkuu wa UN aadhimisha Siku ya Wanawake Papua New Guinea

Amina J Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (katikati kulia) akiungana katika matembezi kuunga mkono siku ya kimataifa ya wanawake huko Port Moresby Papua New Guinea
United Nations/Nahla Valji
Amina J Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (katikati kulia) akiungana katika matembezi kuunga mkono siku ya kimataifa ya wanawake huko Port Moresby Papua New Guinea

Naibu Katibu Mkuu wa UN aadhimisha Siku ya Wanawake Papua New Guinea

Wanawake

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohammed amesherehekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake leo Jumapili huko Port Moresby, Papua New Guinea, na kuzindua mpango wa Spotlight kwa ushirikiano na serikali ya nchi hiyo na Jumuiya ya Ulaya ili kumaliza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Mpango wa Spotlight ni ushirikiano wa kimataifa wa miaka mingi kati ya Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Mataifa unaolenga kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ifikapo 2030.

Papua New Guinea watafaidika na uwekezaji wa dola milioni 22 kwa zaidi ya miaka mitatu ili kutekeleza mpango huo.

Pesa hizo zitaimarisha uwezo wa kutekeleza mkakati wa kupambana na unyanyasaji wa kijinsia, kupanua mipango ya kubadilisha viwango vya kijamii, kuimarisha sekta za haki na ulinzi wa watoto, afya, kuboresha ubora wa takwimu na kusaidia mashirika ya ndani na ya kijamii katika kukabili suala hili.

Mpango wa ufuatiliaji utaundwa kwa ajili ya kazi ngumu ambayo tayari inafanywa na serikali.

Na Umoja wa Mataifa, EU, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, watazingatia uwekezaji mkubwa katika majimbo 11 ya mikoa yote minne ya nchi hiyo. “Kila mtu anapaswa kufaidika na mpango wa Spotlight, moja kwa moja," amesema Naibu Katibu Mkuu katika mkutano na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa mpango huo huko Port Moresby.

Kutekeleza mpango endelevu wa maendeleo

Bi. Mohammed amesisitiza umuhimu wa kuwezesha wanawake na vijana kama sehemu ya juhudi za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

"Hatuwezi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, ajenda ya ulimwengu kwa watu, sayari na ustawi, ikiwa hatutaleta sawa nusu ya idadi ya watu wote duniani. Hatuwezi kusema tumepata amani ikiwa nusu ya jamii zetu zinaishi kwa hofu, ukosefu wa usalama na bila heshima, "amesema.

Naibu Katibu Mkuu katika ziara hiyo huko Papua New Guinea ameambatana na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS, Winnie Byanyima, na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya vijana, Jayathma Wickramanayake.

Wakati wa ziara hiyo ya siku tatu, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umekutana na waziri mkuu na maafisa wengine wa serikali, wawakilishi wa vijana, watetezi wa haki za binadamu, viongozi wa wanawake, na watu wanaoishi na VVU.