Heko wanawake wa Somalia kwa mchango wenu :UNSOM

7 Machi 2020

Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani hapo Machi 8 mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM umewapongeza wanawake wa nchi hiyo kwa jukumu lao katika mchakato wa maendeleo ya nchi hiyo huku ukichagiza juhudi kubwa za kuhakikisha ushiriki wao katika nyanja zote za jamii ya Wasomali.

Akisisitiza mchango wa wanawake hao mkuu wa UNSOM na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia James Swan amesema “wanawake wa Somalia wametoa mchango mkubwa wakati Somalia ikijijenga upya na kuendelea na mwelekeo wa amani na utulivu. Wameonyesha ujasiri mkubwa, ushupavu na kujitoa kimasomaso kukiwa na changamoto kubwa ikiwemo vita vya muda mrefu, kutokuwepo na usalama, majanga ya asili na msukosuko wa kisiasa.”

Ameongeza kuwa, “kwa bahati mbaya changamoto ya usalama kwa wanawake mara nyingi inawafanya kuwa waathirika na mara chache wanachukuliwa kama chachu muhimu katika kuimarisha hali ya usalamakwa wao wenyewe na wengine. Hili ni lazima libadilike.”

Kaulimbiu ya siku ya wanawake mwaka huu ni “Mimi ni kizazi cha usawa” katika kufikia usawa wa wanawake kuelekea uchaguzi mkuu wa Somalia wa mtu mmoja , kura moja , Umoja wa Mataifa nchini Somalia umewataka wadau wote  nchini Somalia hususani uongozi wa kisiasa kuunga mkono uwakilishi wa wanawake katika siasa na kufanya maamuzi na kuhakikisha kwamba usawa unakuwa si ndoto tena bali hali halisi kwa Wasomali wote bila kujali jinsia yao.

Kwa mantiki hiyo Umoja wa Mataifa unaunga mkono kiwango cha chini cha asilimia 30 iliyotengwa kwa ajili ya uwakilishi wa wanawake bungeni. Umoja wa Mataifa pia umechagiza kuendelea kutoa kipaumbele kwaviongozi wa kitaifa kuhusu mswada wa sharia ya uhalifu wa kingono na sharia dhidi ya ukeketaji kama suala muhimu katika kulinda haki za wanawake nchini Somalia.

“Haki sawa kwa wanawake, furs ana ushiriki ni muhimu sana katika kutimiza ajenda ya maendeleo ya Somalia. Na ni juhudi za pamoja pekee zinazojumuisha kila mtu ikiwemo walioko madarakani ndizo zitaweza kufanikisha hili.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud