Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za kijeshi zikome mara moja na bila vikwazo Yemen:UN

Martin Griffiths akizungumza na wanahabari wakati wa ziara yake mjini Marib
Ismini Palla
Martin Griffiths akizungumza na wanahabari wakati wa ziara yake mjini Marib

Operesheni za kijeshi zikome mara moja na bila vikwazo Yemen:UN

Amani na Usalama

Katika ziara yake Kaskazini Mashariki mwa Yemen hii leo Jumamosi mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Martin Griffiths amerejea wito wake wa kusitisha mara moja operesheni za kijeshi na kuzitaka pande kinzani kushirikiana katika kuelekea kukomesha mapigano yanayoendelea.

Bwana. Griffiths ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya siku moja Marib, ambako amekuelezea kama “peponi”wakati mapigano yakiendelea kwingineko baina ya vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na saudia na wapiganaji wa Ansar Allah, ambao pia wanajulikana kama Houthis.  

Melfu ya watu wamefungasha virago na kukimbilia eneo hilo kufuatia mapigano makali katika jimbo jirani la Al Jawf.

“Wiki iliyopiata nilitoa wito kwa umma wa kusitisha operesheni zote za kijeshi. Leo narejea witi huo wa kutaka kusitisha mara moja na bila masharti yoyote operesheni hizo na kuanza mchakato wa kina na jumuishi wa kutekeleza wito huo” amewaambia waandishi wa habari.

Akiwa Marib, Bwana. Griffiths amekutana na gavana wa jimbo hilo na viongozi wa kijamii wa eneo hilo wakiwemo machifu wa kikabila, asasi za kiraia , wanawake, vijana na wakimbizi wa ndani.

“Marib kimekuwa kisiwa cha utulivu ukizingatia vita vinavyoendelea kwingineko. Pande kinzani zinahitaji kuhakikisha kwamba Marib inasalia kuwa peponi na haigeuki kitovu kingine cha machafuko  na vita.”ameongeza bwana.Grifiths

Mwakilishi huyo maalum amesisitiza msimamo wa Umoja wa Mataifa kwamba vita haviwezi kumalizwa kwenye uwanja wa mapambano.

Amesema Yemen iko katika wakati muhimu sana “Ama tutanyamazisha silaha na kuanza mchakato wa kisiasa au tutatumbukia katika zahma kubwa ya vita na madhila ambayo tayari mmeshayashuhudia hapa"