UKIMWI bado unaongoza kwa vifo vya wanawake wenye umri wa kuzaa- UNAIDS

5 Machi 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kutokomeza UKIMWI, UNAIDS, hii leo mjini Geneva Uswisi na Johannesburg Afrika Kusini limezindua ripoti yake mpya ikionesha kuwa kukosekana kwa usawa na fursa sawa kati ya wanaume na wanawake kunaendelea kuwafanya wanawake na wasichana kuwa katika hatari ya Virusi Vya UKIMWI yaani VVU na hivyo gonjwa hilo kusalia kuwa sababu ya kwanza ya vifo miongoni mwa wanawake wenye  umri wa kuzaa, ikiwa ni miak a41 tangu kuanza kwa janga hilo.

Taarifa kuhusu ripoti hiyo iliyotolewa kuelekea Siku ya Kimataifa ya wanawake, imemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima akisema, “janga na VVU linaangazia ukosefu waa usawa na haki vinavyowakabili wanawake na wasichana na jinsi mapungufu katika haki na huduma, vinavyozidishaa janga hili. Hii haikubaliki, inaepukika na inatakiwa kufikia ukomo.”

Miaka 25 iliyopita, serikali zilichukua hatua ya kihistoria ya kupitisha Azimio la Beijing na Jukwaa la kuchukua hatua, mpango mkakati wa kimataifa ulio kamili wa kutimiza haki za binadamu za wanawake na wasichana na kufikia usawa wa kijinsia.

Ripoti ya UNAIDS imefafanua kuwa hatua zimepigwa katika maeneo ya msingi ikitolea mfano, wasichana wengi wako shule na pengo la jinsia katika shule za msingi linapungua duniani kote. Katika baadhi ya nchi kuna wanawake wengi wanaohusika katika uongozi wa kisiasa na nchi nyingine zimefanya kazi kuwalinda haki za wanawake katika sheria. Matibabu ya VVU yameongezeka ambapo kufikia  katikati mwa mwaka 2019 kulikuwa na zaidi ya watu milioni 24 waliokuwa wanaishi na VVU na wakiwa kwenye matibabu wakiwemo wanawake milioni 13 wenye umri wa miaka 15 na zaidi. 

Ripoti hiyo pia inaonesha hata hivyo kuwa ahadi nyingi zilizotolewa kuboresha maaisha ya wanawake na wasichana kote duniani, hazijatekelezwa. Takribani miaka 40 ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu, umesalia kuwa chanzo cha vifo vya wanawake wa kati ya umri wa miaka 15 na 49 na wanawawake wa umri mdogo takribani 6000 wa umri wa miaka 15 hadi 24, wanapata VVU kila wiki.

Ripoti imesema, “tuna maeneo muhimu ya kushughulikia ikiwemo kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake. Katika maeneo ambayo kuna maambukizi makubwa ya VVU, ukatili waa watu waliko katika uhusiano,umeonekana kuongeza hatari ya wanawake kupata VV kwa asilimia 50. Kuwa na VVU kunaweza pia kuchochea vurugu, ambapo wanawake wanaoishi na VVU wamekuwa maara kwa mara wakiripoti kufanyiwa ukatili kutoka kwa wenza wao, familia na wanajamii na pia katika huduma za afya.”

Ripoti imeeleza hatua kadhaa za kuchukuliwa ili kusonga mbele ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika sera na programu za VVU ambazo zimethibitisha kukuza usawa wa kijinsia, kuwekeza katika elimu, ikiwemo elimu thabiti ya afya ya uzazi na uwezeshaji wanawake na wasichana kiuchumi, kurekebisha sheria ambazo zinakawamisha haki sawa kwa wanawake na wasichana wote ikiwemo hatua za kukomesha unyanyapaa na ubaguzi, unyanyasaji na uhalifu unaoelekezwa kwa wanawake na wasichana.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud