Pérez  de Cuéllar ameacha alama chanya duniani - Guterres

Mchoro wa Katibu Mkuu wa tano wa Umoja wa Mataifa,Javier Pérez  de Cuéllar
UN Photo/Manuel Elías
Mchoro wa Katibu Mkuu wa tano wa Umoja wa Mataifa,Javier Pérez de Cuéllar

Pérez  de Cuéllar ameacha alama chanya duniani - Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa Javier Pérez  de Cuéllar amefariki dunia. Alikuwa na umri wa miaka 100.

De Cuéllar raia wa Peru ambaye amefariki dunia Jumatano ya Machi 04, alihudumu mihula miwili kwenye Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe  1 Januari mwaka 1982 hadi tarehe 31 Desemba mwaka 1991.

Kufuatia taarifa za kifo chake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa taarifa kupitia msemaji wake akieleza masikitiko  yake makubwa kufuatia kifo cha de Cuéllar.

“Alikuwa mwanasiasa mzoefu, mwenye stadi na mwanadiplomasia aliyejizatiti na mtu ambaye aliacha alama kubwa kwenye Umoja wa Mataifa na duniani kote,” amesema Guterres kwenye taarifa yake hiyo.

Ameenda mbali akisema kuwa maisha ya Pérez de Cuéllar yamekuwa ya siyo tu karne moja bali pia historia nzima ya Umoja wa Mataifa kuanzia ushiriki wake katika mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1946.

Guterres amesema kipindi chake cha  uongozi akiwa Katibu Mkuu kiliendana na zama mbili muhimu ambazo ni mosi, “baadhi ya miaka migumu ya vita baridi na hatimaye mzozano wa kiitikadi , kipindi ambacho Umoja wa Mataifa ulianza kutekeleza kwa dhati dhima iliyobuniwa na waasisi wa umoja huo.”

Katibu Mkuu Javier Perez de Cuella akizuru kundi la mpito la msaada (UNTAG) kwenye makao yake makuu ya jeshi nchini Namibia 1989
UN Photo/Milton Grant
Katibu Mkuu Javier Perez de Cuella akizuru kundi la mpito la msaada (UNTAG) kwenye makao yake makuu ya jeshi nchini Namibia 1989

Mizozo aliyokabiliana nayo

Pérez de Cuéllar alikuwa na dhima muhimu katika maeneo muhimu yaliyokuwa ni mafaniki kidiplomasia ikiwemo uhuru wa Namibia, kumalizika kwa vita kati ya Iraq na Iran, kuachiliwa huru kwa mateka wa kimarekani waliokuwa wakishikiliwa nchini Lebanon, mkataba wa amani nchini Cambodia na katika siku zake za mwisho kabisa ofisini mkataba wa amani wa kihistoria nchini El Salvador.

Katibu Mkuu ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Pérez de Cuéllar, wananchi wa Peru na watu wengine wengi duniani kote ambao maisha yao yaliguswa na kiongozi huyo wa kimataifa ambaye ameaga dunia na kuiacha pahala bora zaidi.

Safari hadi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

De Cuéllar ambaye kitaaluma alikuwa mwanasheria, tangu mwaka 1940 katika maisha yake alishika nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia kuanzia kwenye wizara ya mambo ya nje na kwenye Umoja wa Mataifa.

De Cuéllar aliwahi kuwa balozi wa Peru nchini Uswisi, Kwenye Muungano wa kisovieti, Poland na Venezuela.

Kama miongoni mwa wajumbe wa Peru alishiriki kikao cha kwanza cha Baraza Kuu mwaka 1946. Na akawa mwakilishi wa kudumu wa Peru kwenye Umoja wa Mataifa mwaka 1971 na kuanzia hapo ni kama hakuondoka kwenye Umoja wa Mataifa.

Mwaka 1975 De Cuéllar aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Cyprus na kushika nyadhifa nyingine mbalimbali mpaka Desemba 1977 na miaka miwili baadaye alichukua wadhifa wa msaidizi maalum wa Katibu Mkuu kwenye masuala ya kisiasa.

Na kuanzia Aprili mwaka 1981 alihudumu kama mwakilishi wa Katibu Mkuu katika kutatua mgogoro wa Afghanistan na hata aliporejea kufanyakazi kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Peru, Pérez  de Cuéllar aliendelea kumwakilisha Katibu Mkuu katika masuala ya Afghanistan.

Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa UN akiwa na Mama Teresa Oktoba 1985
UN Photo/John Isaac
Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa UN akiwa na Mama Teresa Oktoba 1985

Wadhifa wa juu zaidi UN

Baada ya kuchukua madaraka rasmi kama Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa tarehe 1 Januari 1982, miezi michache baadaye katika ripoti yake ya kwanza kuhusu kazi za shirika kiongozi huyo alitoa tathimini iliyokosoa vikali , kwa mujibu wake wakati huo Baraza la usalama “haliwezi kuchukua maamuzi ya hatua za lazimakutatua migogoro ya kimataifa. Na hata maamuzi hayo yanapofanyika matarajio ya utekelezaji wake katika mazingira ya mgawanyiko kwenye jumuiya ya kimataifa ni sifuri.”

Kipaumbele chake kilikuwa kuubadilisha Umoja wa Mataifa kuwa shirika linaloweza kutimiza majukumu yake ya kuhakikisha amani na usalama. De Cuéllar alisema “endapo hili halitofanyika jumuiya ya kimataifa itakuwa kazi bure katika masuala ya migogoro ya kijeshi ambayo inatishia msingi wa amani ya kimataifa.”

Akiondoka madarakani katika majira ya kiangazi mwaka 1991 de Cuéllar alitoa ripoti yake ya mwisho ambayo ilikuwa tofauti na ya kwanza safari hii aliandika kuhusu kufufua Umoja wa Mataifa, kumaliza mkwamo wa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa 5 “Umoja wa Mataifa ulikuwa ukienda sanjari na mabadiliko ya haraka ya kihistoria katika miaka ya karibuni na ulipata mafanikio makubwa katika ulinzi wa mani.” 

Licha ya kukosolewa hapa na pale mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema “hakuna mtu anayeweza kuongeza mara mbili utendaji wa Umoja wa Mataifa . Umoja wa Mataifa unaingia katika zama mpya na unachukua majukumu ambayo hayakuwepo kwenye mipango ya awali ya kuanzishwa kwa umoja huu.”