Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa Tanzania na UN Kigoma waleta nuru kwa  manusura wa ukatili wa kijinsia

Evans Siangicha, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Programu ya pamoja ya Kigoma akihojiwa mjini Kigoma.
UN News/Assumpta Massoi
Evans Siangicha, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Programu ya pamoja ya Kigoma akihojiwa mjini Kigoma.

Ushirikiano wa Tanzania na UN Kigoma waleta nuru kwa  manusura wa ukatili wa kijinsia

Wahamiaji na Wakimbizi

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma, KJP, inayotekelezwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa imeweza kuleta chachu katika mpango wa taifa wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Mratibu wa programu hiyo mkoani humo Evans Siangicha akihojiwa na Assumpta Massoi wa UN News Kiswahili hivi karibuni mjini Kigoma amesema kipengele hicho kinachotekelezwa katika makundi matatu ambacho cha kwanza ni kuboresha mfumo uliopo kwa kuongeza wataalamu ambao awali walikuwa wachache, “programu hii imeweza kuongeza wataalamu 18 ambao wanalipwa mishahara na kila kitu kutokana na ufadhili wa programu. Pia kutoa usaidizi kwa waathirika kupitia kutoa mafunzo kwa maafisa polisi na maafisa wa usawa wa jinsia waliopo na pia kujenga madawati ya jinsia. Mpaka sasa programu imejenga madawati ya jinsia manne katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Kigoma na Kasulu. Yote yameanza kufanya kazi.”

Halikadhalika amesema wanaelimisha umma kuhusu madhara ya unyanyasaji wanawake na watoto na pia, “tunajishughulisha na kuweka vituo ambavyo ni salama kwa wale wahanga, ambao wakati matatizo yao yanashughulikiwa wanaweza kusaidiwa kwa kipindi matatizo  yao yanashughulikiwa. Kuna familia salama ambazo zimeteuliwa na kupatiwa mafunzo,na zinasaidiwa na zinaweza kukaa na watoto wenye shida mbalimbali  lakini pia kuna kituo ambacho kinaitwa nyumba salama ambacho  kiko Kasulu na kinachukua waathirika mbalimbali wa masuala  haya.”

Kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa kike ni miongoni mwa maeneo 7 ambayo kupitia mradi wa pamoja wa Kigoma mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa yanashirikiana kuyaboresha kwenye wilaya Kibondo, Kakonko na Kasulu mkoani Kigoma ambako kuna kambi za wakimbizi.

Maeneo mengine ni elimu kwa wasichana na wanawake wadogo, maji, kilimo, nishati endelevu, kuwezesha wanawake na vijana pamoja na afya,  ukimwi na lishe ambalo liliongezwa mwaka jana wa 2019.

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.