Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Virusi vya Corona vyatikisa uchumi wa dunia, uzalishaji China wasinyaa- UNCTAD

Mwanamke katika kiwanda cha kutengeneza wanasesere, Shenzen, China.
Unsplash/Carl Nenzen Loven
Mwanamke katika kiwanda cha kutengeneza wanasesere, Shenzen, China.

Virusi vya Corona vyatikisa uchumi wa dunia, uzalishaji China wasinyaa- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamati ya  maendeleo ya biashara ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, imesema virusi vya Corona au COVID-19, vimesababisha uzalishaji nchini China kusinyaa kwa asilimia 2 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

UNCTAD imesema hayo leo kupitia chapisho lake kuhusu athari virusi vya Corona kwa biashara duniani ambalo limechambua athari za kiuchumi, chapisho ambalo limetolewa huko Geneva, Uswisi.

“Katika miongo miwili iliyopita, China imekuwa muuzaji mkubwa wa bidhaa zake nje ya nchi na kuwa sehemu ya mtandao mkubwa wa uzalishaji duniani. China imejiweka kuwa mtoaji muhimu wa malighafi muhimu za bidhaa nyingi kuanzia magari, simu za kiganjani, vifaa vya matibabu na vingine vingi,”  imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo ripoti imesema katika mwezi mmoja uliopita, China imeshuhudia anguko kubwa la kipimo chake cha uzalishaji hadi 37.5, kiwango ambacho ni cha chini zaidi tangu mwaka 2004.

“Anguko hilo linamaanisha kuwa kupungua kwa asilimia 2 katika uzalishaji kwa mwaka, na hii ni madhara ya moja kwa moja ya kusambaa kwa virusi vya Corona,”  imesema ripoti hiyo.

UNCTAD  inasema kuwa kusinyaa kwa uzalishaji wa China kwa asilimia 2 kuna athari hasi kwenye uchumi wa dunia na hadi sasa imesababisha hasara ya dola bilioni 50 katika mataifa mbalimbali.

Sekta zilizoathirika zaidi ni zile za vifaa vya vipimo, mashine, magari na mawasiliano huku nchi ambazo zimeguswa zaidi ni zile za Muungano wa Ulaya, Marekani, Japan, Korea Kusini na Vietnam.

Kamati hiyo imeonya kuwa hata kama mlipuko wa virusi vya Corona utadhibitiwa ndani ya China, suala kwamba wasambazaji wa bidhaa wa China wana umuhimu mkubwa sana kwa kampuni nyingi duniani, ina maana kwamba “zahma yoyote nchini China inaweza kutikisa minyororo ya usambazaji wa bidhaa nje ya mipaka na kuathiri Ulaya, Amerika na Asia ya Mashariki.

Meli ya mizigo ikiwa na shehena yake kwenye bandari ya Ningbo, China
IMO
Meli ya mizigo ikiwa na shehena yake kwenye bandari ya Ningbo, China

Makadirio ya hasara kiuchumi

Akichambua ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Pamela Coke-Hamilton, ambaye in Mkuu wa kitengo cha biashara ya kimataifa na bidhaa, UNCTAD amesema kuwa nchi zinazotarajiwa kuathirika zaidi ni zile za Muungano wa Ulaya, EU, zikitarajiwa kupoteza dola bilioni 15.5, Marekani dola bilioni 5.8, Japan dola bilioni 5.2.

“Kuhusu chumi zinazoendelea ambazo ni tegemezi kwa kuuza malighari, athari zitakuwa kubwa mno,” amesema Bi. Coke-Hamilton akiongeza kuwa kwa kutazamia kuwa madhara hayo hayawezi kupunguzwa katika kipindi kifupi, “kuna uwezekano kuwa kwa jumla athari katika uchumi wa dunia inaweza kuwa dhahiri kwa kuporomoka.”

Naye Alessandro Nicita, kutoka kitengo cha biashara ya kimataifa na bidhaa, amesema, “bila shaka, iwapo virusi hivyo vitaendelea kusambaa na kushindwa kudhibitiwa, tutaona viwanda vikifungwa siyo tu  nchini China, bali pia India na Marekani na kwingineko duniani na hiyo itakuwa tatizo kubwa.”

Hata hivyo amesema madhara ya kiuchumi yanategemea hatua zinazochukuliwa na kila nchi kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

“Kwa mantiki hiyo, China imefanya kazi nzuri sana ya kudhibiti virusi, lakini kwa kiasi kikubwa imegharimika kiuchumi, angalau kwa wiki za mwanzoni,”  amesema Bwana Nicita akiongeza kuwa, “kwa hiyo mipango ya kufunga viwanda, udhibiti wa mienendo ya watu,  vyote vilikuwa muhimu, lakini kuna athari za kiuchumi zitokanazo na hatua hizo.”

Shehena za kontena nazo zapungua

Pamoja na kuporomoka kwa kiwango cha uzalishaji, UNCTAD imeangazia pia kupungua kwa idadi ya kontena zinazosafirishwa kwa meli kutoka bandari ya Shanghai, katika nusu ya kwanza ya mwezi Februari.

Idadi hiyo imepungua kutoka kontena 300 kwa wiki hadi kontena 181, kiwango ambacho  kilirejea katika hali ya kawaida nusu ya pili ya mwezi huo wa Februari.

Bi. Coke-Hamilton amesema kuwa kwa hivi sasa madhara ya virusi hivyo kwenye mnyororo wa thamani duniani tayari umedhihirika, lakini “utaweza kuendelea kwa miezi michache ijayo na kwamba iwapo hali itakwamuka miezi michache ijayo, basi madhara ya muda mrefu au mwaka mzima yatakuwa tofauti au yatakuwa nafuu. Kwa hiyo inategemea na kile kinachoendelea China.”

Je nchi zitafute wazalishaji wengine wa bidhaa na malighafi?

Walipoulizwa kuhusu iwapo nchi zinaweza kuchukua hatua za kupunguza madhara kwa kutafuta wazalishaji wengine wa malighafi hata kusaka wazalishaji hao ndani  ya nchi, wachumi hao wa UNCTAD wamesema kuwa hatua kama hiyo haitakuwa na manufaa katika kipindi kifupi.

Bwana Nicita amefafanua kuwa, “China imejenga mifumo mikubwa ya usafirishaji na uzalishaji kama vile bandari, meli za kusafirisha mizigo, ndege ambazo zinaweza kuingiza na kutoa bidhaa zote kwenda na kutoka China.”

Ameongeza kuwa, hivi sasa baadhi ya viwanda vinaweza kutafuta wasambazaji wa wengine kutoka Mexico au Ulaya Mashariki, “lakini hiyo itahitaji muda zaidi, kwa sababu siyo tu miundombinu ya uzalishaji inapaswa kuhamishwa, bali pia miundombinu inayohusika na usafirishaji wa bidhaa na hiyo itapaswa kujengwa.”

Akifafanua zaidi, Bi. Coke-Hamilton amesema kuwa, “ni hoja hiyo ambayo Rais wa Marekani alidhania kuwa kwa kuweka mikakati fulani kwa nchi fulani, kunaweza kusaidia kurejesha viwanda vya uzalishaji bidhaa nchini Marekani. Katu si rahisi hivyo, kwa sababu pindi kampuni zinapohama na kuhamisha miundombinu yake na kuanzisha viwanda vyao na mifumo ya usafirishaji, inakuwa vigumu kuihamisha katika muda mfupi.”

Shirika la afya duniani, WHO lilitangaza kuwa virusi vya Corona ni dharura ya afya ya umma duniani tarehe 30 mwezi Januari mwaka huu, huku China ikiwa imeripoti wagonjwa mwezi Desemba.