Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC imepiga hatua kubwa katika kudhibiti Ebola:WHO

Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Thomas Nybo
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

DRC imepiga hatua kubwa katika kudhibiti Ebola:WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema kuna hatua kubwa imepigwa katika kudhibiti mlipuko wa ebola nchini Jamhuri ya Kimekrasia ya Congo DRC, huku visa vikipungua kutoka 120 kwa wiki mwezi mwaka jana hadi visa vidatu au sufuri kwa wiki nne zilizopita

Katika kitovu cha mlipuko wa Ebola mjini Beni, mpango ulioanzishwa na WHO kwa kushirikiana na wizara ya afya ya DRC unarahisisha kazi ya ufuatiliaji wa watu wanaosemekana kukutana na wagonjwa wa Ebola.

Mpango huu ni wa kuwapa chaguo la kuishi kwenye nyumba maalum za wageni kwa siku 21, watu wanaoonekana kuwa katika hatari ya maambukizi ili wafuatiliwe kwa karibu.

Na katika nyumba hizi wanapewa chakula na kupimwa kila siku. Mtazamo huu umewawezesha watu kwenda kwenye vituo vya afya mara moja baada ya kuona dalili na hivyo kupunguza hatari ya maambukizi kwenye jamii kama anavyosema Papy Musa mratibu wa WHO Beni,“tumekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu hapa ni rahisi kuwabaini watu waliothibitishwa kuwa na ebola kwa wakati na kuwapeleka kwenye vituo vya Ebola, jinsi mtu anavyobainika mapema ndivyo anavyokuwa na fursa kubwa ya kupona.”

Watu wanaoamua kukaa kwenye vituo hivyo vya ufuatiliaji wanafanya hivyo kwa hiyari yao na baada ya kuelimishwa. Zoe Kyavanhandi ni afisa mawasiliano wa WHO katika moja ya vituo hivyo vya ufuatiliaji,“ninawaonyesha hatari iliyopo, kisha wanafanya maamuzi , wanakuja na kukaa hapa nasi na hivyo tunawafuatilia na kujaribu kudhibiti watu wanaokutana nao.”

Ameongeza kuwa wengi wao wanaelewa umuhimu akiwemo Doti Kavugho shangazi wa mmoja wa wagonjwa wa Ebola

WHO inasema wengi wa watu hawa wanapoondoka kituoni wanakuwa mabalozi wazuri wa kuchagiza usafi na kujikinga na Ebola.