Timu ya WHO yawasili Tehran ili kuisaidia Iran kupambana na COVID-19

2 Machi 2020

Timu ya wataalam wa shirika la afya duniani WHO imewasili mjini Tehran ili kuisaidia nchi ya Iran katika juhudi zinazoendelea za kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19) nchini humo.

Timu hiyo itafanya kazi kwa karibu na mamlaka za afya na wadau wengine kutathimini juhudi zinazoendelea za hatua za kupambana na ugonjwa huo, kuzuru vituo maalum vya afya, maabara na maeneo ya mipakani ya kuingia na kisha kutoa muongozo wa kiufundi.

Kwa ujumla lengo la ziara hiyo ni kubaini mwenendo wa maambukizi na hatari kwa umma, kutoa muongozo wa kuimarisha na kuongeza juhudi za kupambana na mlipuko unaoendelea, ikiwemo makubaliano ya hatua za kipaumbele za kudhibiti mlipuko na kutoa muongozo kuhusu kuimarisha udhibiti katika maeneo ambayo bado hayajaathirika na mlipuko huo.

Hadi kufikia leo kuna visa 1501 vya COVID-19 vilivyothibnitishwa nchini Iran ikiwemo vifo 66. Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya afya ya Iran watu 291 tayari wanatuhusiwa kutoka hospitali baada ya kupona.

Visa vinavyotokana na historia ya kusafiri kwenda Iran vimeripotiwa kutoka Afghanistan, Canada, Lebanon, Pakistan, Kuwait, Bahrain, Iraq, Oman, Qatar na Emarati.

Ndege iliyowabeba timu ya wataalam hao pia ilijumuisha madawa na vifaa tiba, ikiwemo vifaa vya kujikinga kuwasaidia zaidi ya wahudumu wa afya 15,000 pamoja na vifaa vya kutosha vya maabara ambavyo vinaweza kuwapima karibu watu 100,000.

WHO imeishukuru serikali ya Emarati kwa kutoa ndege hiyo ambayo imeiwezesha WHO kupeleka timu na vifaa tiba nchini Iran.

TAGS:WHO, Iran, COVID-19, Emarati,

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud