Asante Ujerumani kwa Euro milioni 17 za kukabiliana na nzige:FAO
Asante Ujerumani kwa Euro milioni 17 za kukabiliana na nzige:FAO
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO, QU Dongyu amekaribisha msaada wa Euro milioni 17 kutoka kwa serikali ya Ujerumani ili kutoa msaada wa moja kwa moja kwa waathirika wa janga la nzige Afrika Mashariki.
Tangazo la msaada huo limetolewa leo na mwakilishi wa kudumu wa Ujerumani kwenye shirika la FAO mjini Roma Italia na msaada huo ni nyongeza kwani Ujerumani tayari imeshachangia Euro milioni 3 kwa ajili ya janga hilo.
Akikaribisha msaada huo mkurugenzi wa FAO Bwana. Qu amesema, “nataka kuishukuru serikali ya Ujerumani kwa usamaria na mchango wake na kwa kutambua haja ya haraka ya kukabiliana na athari mbayá za mlipuko huu wa nzige. Tunafanya kila juhudi kudhibiti kusambaa zaidi kwa nzige hao na pia kulinda maisha na kuchagiza watu kujikwamua tena nakutoka kwenye janga hili.”
Kwa mujibu wa FAO huu ni mlipuko mbaya zaidi kuwahi kulikumba eneo hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 25 na Kenya haijawahi kushuhudia tatizo kubwa kama hili kwa miaka 70. Shirika hilo limeongeza kuwa maeneo mengine yaliyoripotiwa kukumbwa na nzige ni Sudan Kusini na Uganda ingawa huko hali si mbayá sana.
Maeneo zaidi yako katika hofu
Wiki hii FAO inasema mazalia mapya yameonekana Bahrain, Kuwait, Saudia, Qatar na Jamhuri ya Iran.
Mkurugenzi wa FAO amesisitiza kwamba hali ni mbaya zaidi Afrika Mashariki ukanda ambao watu milioni 20 tayari wanachukuliwa kuwa hawana uhakika wa chakula. Bwana Qu ameongeza kuwa “kupambana na nzinge ni nusu ya vita vyetu , nusu nyingine ni kusaidia watu walioathirika hivyoi msaada wa Ujerumani utaliwezesha shirika la FAO kutoa msaada unaohitajika kuwasaidia wakulima na familia zao.”
FAO imetoa ombi la haraka la dola milioni 138 kwa ajili ya kuzisaidia nchi ambazo zimeathirika na tangazo la mchango zaidi wa fedha kutoka Ujerumani utafanya ahadi ya fedha za msaada iliyotolewa na wahisani kufikia dola milioni 69.
Kati ya dola hizo milioni 138 zilizoombwa zaidi ya dola milioni 60 zitatumika kukabiliana na kusambaa kwa maradhi, zaidi ya dola milioni 67 kulinda maisha na kujikwamua kutoka katika janga hilo na karibu dola milioni 10 zitatumika kuchagiza uratibu wa kikanda na maandalizi.