Skip to main content

Sote tuone aibu kwa ukosefu wa usawa wa wanawake karne ya 21 - Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akieleza kuhusu kujitolea kwake kwa ajili ya usawa wa kijinsia alipokuwa katika Chuo Kikuu cha The New School mjini New York Marekani
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akieleza kuhusu kujitolea kwake kwa ajili ya usawa wa kijinsia alipokuwa katika Chuo Kikuu cha The New School mjini New York Marekani

Sote tuone aibu kwa ukosefu wa usawa wa wanawake karne ya 21 - Guterres

Wanawake

Karne ya 21 inatakiwa kuwa karne ya usawa wa wanawake, ni kauli iliyotolewa hii leo alhamis na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipokuwa akitoa wito wa kuibadilisha dunia katika kuhakikisha ushiriki sawa kwa wote.

Akiwahutubia wanakitivo na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha New School jijini New York Marekani, Katibu Mkuu Guterres amejitangaza mwenyewe kuwa ni mwanaharakati wa haki za wanawake anayejivunia na akatoa wito kwa wanaume kila mahali kuunga mkono haki za wanawake.

“Kama ilivyo utumwa na ukoloni ulivyokuwa doa katika karne zilizopita, wote tunatakiwa kuona aibu kutokana na ukosefu wa usawa wa wanawake katika karne ya 21. Kwasababu siyo tu haukubaliki, bali pia ni ujinga.” Amesisitiza Bwana Guterres.

Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana vinasalia kuwa dhulma kubwa ulimwenguni, “kutokuwepo kwa usawa na ubaguzi ni desturi ambazo bado ziko kila mahali. Maendeleo yamezorota kwa kiasi cha kukwama na katika mazingira mengine yamerudi nyuma. Kuna msukumo wa nguvu wa kurudisha nyuma haki za wanawake. Ukatili dhidi ya wanawake, ikiwemo mauaji dhidi ya wanawake yako katika viwango vya janga. Na zaidi ya mwanamke mmoja kati ya watatu atakumbana na ukatili wa namna fulani katika maisha yake.”

Aidha Bwana Guterres ametoa ushauri kuwa hivi sasa ni wakati wa kuacha kujaribu kuwabadilisha wanawake na badala yake kuanza kuibadili mifumo ambayo inawazuia wanawake kuweza kuuufikia uwezo wao. Na kwa msingi huo karne ya 21 inapaswa kuwa karne ya usawa wa wanawake.

Vilevile Bwana Guterres amesisitiza mwelekeo wa taasisi anayoiongoza akisema, “wakati Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75, unachukua hatua kubwa kuunga mkono haki za wanawake.”