Mawaziri wa Afya jibuni maswali haya muone iwapo mpo tayari kudhibiti Corona

27 Februari 2020

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limeorodhesha maswali ambayo kila nchi inapaswa kujiuliza ili iweze kufahamu iwapo imejiandaa vyema kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 ama la.

Mkurugenzi Mkuu wa  WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus ametaja maswali hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi katika mkutano wake wa kila siku kuhusu mwenendo wa mlipuko wa virusi vya Corona, ambapo idadi ya wagonjwa wapya kila uchao ni kubywa nje ya China kwa siku mbili mfululizo.

Maswali ya kujiuliza

 1. Je tupo tayari kwa mgonjwa wa kwanza? Je tutafanya nini iwapo tunapata mgonjwa wa kwanza?
 2. Je tuna kitengo cha karantini kwa wagonjwa? Je tuna oksijeni ya kutosha, vifaa vya kusaidia kuvuta pumzi na vifaa vingine muhimu?
 3. Je tutafahamu vipi iwapo kuna wagonjwa kwenye maeneo mengine ya nchi?
 4. Je kuna mfumo wa kutoa taarifa ambao vituo vya afya unatumia na mbinu pia ya kutoa tahadhari iwapo kuna hofu?
 5. Je wahudumu wetu wa afya wana mafunzo na vifaa wanavyohitaji ili wawe salama?
 6. Je wahudumu wa afya wanafahamu jinsi ya kuchukua sampuli ya uchunguzi kutoka kwa wagonjwa?
 7. Je katika viwanja vya ndege na  mipakani tuna mikakati ya kuchunguza watu iwapo ni wagonjwa?
 8. Je maabara zetu zina vitendanishi vya kuwezesha kuchunguza sampuli?
 9. Je tuko  tayari kutibu wagonjwa walio mahututi?
 10. Je  hospitali zetu na kliniki zina kanuni sahihi za kukinga na kuzuia maambukizi?
 11. Je wananchi wa taarifa sahihi? Je wanafahamu dalili za ugonjwa husika? Ya kwamba si mafua bali katika asilimia 90 ya wagonjwa ni homa na asilimia 70 ni kikohozi kikavu.
 12. Je tuko tayari kukabili uvumi na taarifa potofu kwa kutoa ujumbe ambao ni rahisi kwa wananchi kuelewa?
 13. Je tuko tayari kwa wananchi wetu kukabiliana na mlipuko?
National Institute of Allergy and Infectious Diseases, NIH, US
Picha ya rangi ikionyesha seli ambayo imekumbwa na virusi vya MERS-Corona

 

Dkt. Tedros amesema maswali hayo 13 ni ambayo kila Waziri wa Afya anapaswa kuwa tayari kuyajibu na kwamba, “ maswali haya yataweza kuonesha tofauti kubwa kati ya mgonjwa 1 na wagonjwa 100 katika siku na wiki chache zijazo.”

Idadi ya wagonjwa hivi sasa duniani.

Nje ya China hadi leo hii Alhamisi kuna wagonjwa 3474 katika nchi 44 na vifo ni 54.

Katika saa 24 zilizopita, nchi 7 zimeripoti visa kwa mara ya kwanza nazo ni; Brazil, Georgia, Ugiriki, Macedonia Kaskazini, Norway, Pakistan na Romania.

Dkt. Tedros amesema hakuna nchi yoyote ambayo inaweza kujihakikishia kuwa haitaweza kupata COVID-19, “hilo litakuwa ni kosa kubwa. Virusi hivi haviheshimu mipaka. Virusi hivi havitofautishi kati ya rangi ya mtu au kabila. Havitambua pato la ndani la taifa au kiwango cha maendeleo.”

Amesema kuwa dunia haipaswi kupoteza matumaini na kuacha kujikinga, bali kila nchi ina wajibu wa kuchukua.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud