Uraibu wa madawa ya kulevya na pombe kwa watoto na barubaru watia hofu

Mvulana mwenye  umri wa miaka 19 akiwa ameketi kitandani kwake kwenye makazi ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu huko Odessa, Ukraine.Kijana huyu anatumia madawa na anaishi na VVU. Lakini hana uwezo wa kupata dawa.
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Mvulana mwenye umri wa miaka 19 akiwa ameketi kitandani kwake kwenye makazi ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu huko Odessa, Ukraine.Kijana huyu anatumia madawa na anaishi na VVU. Lakini hana uwezo wa kupata dawa.

Uraibu wa madawa ya kulevya na pombe kwa watoto na barubaru watia hofu

Afya

Bodi ya kimataifa ya kuzuia madawa ya kulevya INCB imezitaka serikali kuanzisha mifumo ya kitaifa ya data ili kufuatilia mwelekeo wa matumizi ya madawa yenye uraibu miongoni mwa vijana.

Wito wa bodi hiyo umo  katika ripoti yake ya mwaka 2019 iliyotolewa leo  ikiangazia uhusiano kati ya matumizi ya pombe na tumbaku na madawa mengine yenye uraibu kama vile bangi na Cocaine miongoni mwa watoto na barubaru.

Bodi hiyo imesema kuwa uwepo wa mfumo huo utawezesha kuwa na mipango ya kinga inayozatia tafiti na shuhuda, mipango ambayo inaweza kutekelezwa kipindi ambacho mtoto au barubaru hajaanza kutumia madawa hayo.

Kipindi hicho kwa mujibu wa ripoti hiyo ni, kabla ya kuzaliwa, mtoto akiwa mchanga, miaka katiya 5 hadi 10 na wakati kabla ya ubarubaru.

Rais wa Bodi hiyo Cornelis P. de Joncheere, amenukuliwa kwenye ripoti hiyo akisema kuwa, mara nyingi, matumizi ya pombe na tumbaku hutangulia matumizi ya bangi na madawa mengine yanayodhibitiwa. Tafiti ambazo zimefuatilia watoto hadi utu  uzimani zimedhihirisha kuwa pindi mtoto anapoanza kutumia pombe, tumbaku na bangi wakati akiwa na  umri wa miaka 16 hadi 19, basi kuna uwezekano mkubwa ya kwamba akiwa mtu mzima atatumia afyuni na kokeini.”

Kwa mantiki hiyo, INCB kwa kushirikiana na shirika la afya ulimwenguni, WHO wamependekeza mambo yanayopaswa kuwepo kwenye mikakati hiyo ya kuzuia inayotakana na shuhuda dhahiri.

Mosi, uzingatie familia na stadi za malezi, kuhamasisha ushiriki chanya katika maisha ya watoto, mbinu thabiti za mawasiliano ikiwemo kuweka kanuni.

Pili, mitaala ya shule isaidie kuimarisha stadi binafsi na za kijamii za wanafunzi ikiwemo jinsi ya kufanya maamuzi na kuweka malengo ya maisha ili waweze hata kukataa matumizi ya madawa yenye uraibu.

Tatu, ushirikishaji wa shule katika kuchunguza na kutathmini matumizi na hata kutoa ushauri nasaha na ufuatiliaji.

Nne ni kusimamia sheria ili kudhibiti kiwango cha matumizi ya bidhaa za uraibu kama vile tumbaku, pombe na bangi miongoni mwa watoto na barubaru.

INCB imependekeza pia “serikali ziwekeze kwenye maendeleo ya utalaamu kwenye nyanja ya matumizi ya madawa ya kulevya, kinga na matibabu kwa kumulika zaidi vijana. Hii inapaswa kujumuisha mafunzo ya kitaifa na kuwapatia leseni watendaji wote wanaohusika na utoaji wa maamuzi, uandaaji na utekelezaji wa mipango kuhusu madawa ya kulevya.