Radio Okapi yatimiza miaka 18, yafananishwa na kito cha thamani

25 Februari 2020

Radio Okapi ambayo ni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO leo imetimiza miaka 18 tangu kuanzishwa kwake ambapo viongozi mbali mbali wameipongeza kwa siyo tu ueledi wa wafanyakazi wake bali pia kuwa sauti ya wananchi wa taifa hilo la Maziwa Makuu.

Miongoni mwa waliozungumzia maadhimisho hayo ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Bi. Leila Zerrougui ambaye amefaninisha kituo hicho na kito cha thamani akisema kuwa, “tunasherehekea miaka 18 ya Radio Okapi, kwa hiyo basi ningependa kusisitiza umuhimu wa radio hii, umuhimu wa dhima yake katika nchi hii. Kutokana na uwepo wenu, radio hii imekuwa mhimili mkuu wa mawasiliano wa Umoja wa Mataifa, lakini pia ikipaza sauti  za wananchi wa DR Congo kwa sababu hatimaye ni nyinyi wana DR Congo ambao mko wengi, waandishi wa habari huko mashinani ambao katika nyakati ngumu mmekuwa mkikumbwa na matatizo kwa sababu mko kwenye radio hii.”

Ameenda mbali na kusema kuwa, “kwenu ninyi wakati mwingine haikuwa rahisi kufanya kazi kwenye nchi yenu. Lakini tuliwaomba msalie kwenye Umoja wa Mataifa na hii si kila wakati ni rahisi. Nafahamu hata wakati mwingine nilikuwa na msimamo mkali dhidi yenu lakini lengo lilikuwa ni kulinda chombo hiki. Ni chombo hiki ambamo tafiti zote, namaanisha tafiti za vyombo vya habari DR Congo, Radio Okapi inasalia kuwa tunu na tutaendelea kuitunza na kuiendeleza. Hongerezani kwa sikukuu. “

Katibu Mkuu wa  UN  António Guterres akihojiwa na Radio Okapi tarehe 9 Februari mwaka 2019 wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Radio Okapi/Ph. John Bompengo
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihojiwa na Radio Okapi tarehe 9 Februari mwaka 2019 wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa DRC Acacia Bandubola ametaka kituo hicho kizingatie ueledi akitumia msemo wa DRC wa kuwa Radio Okapi iwe sawa na kanisa katikati ya kijiji akisema, “miaka 18 ni kijana mkubwa ni msichana mkubwa ambaye ni mtu mzima. Ni kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, unakuwa mtu mzima ukitimiza umri wa miaka 18. Kwa hiyo mmekomaa leo hii na nawatakia sherehe njema ya kazi nzuri na mfanye kazi kwa amani. Mnakwenda mbali sana kugusa maisha ya wananchi wetu. Mnakwenda  ndani sana na nadhani hata nje ya nchi. Na nawatia moyo muendelee, na mfike hata vijijini muwe mhimili wa nne na kufanya kazi yenu kwa ueledi. Na nawaombe muendelee kuwapatia taarifa wananchi wa DR Congo, taarifa za kweli na nzuri kwa sababu wananchi wa DR Congo, wanahitaji. Hongereni kwa sikukuu.”

Wakati wa mashambulizi na magonjwa Radio Okapi imekuwa sauti  yetu- Bwanakwa

Tathmini pia ya miaka 18 ya Radio Okapi imetolewa na  Meya wa mji wa Beni jimbo la Kivu Kaskazini, Bwana  Nyonyi Bwanakwa ambaye amesema kuwa, “unafahamu ukosefu wa usalama umetanda kuanzia mashambulizi kutoka waasi wa ADF au vikundi vilivyojihami vya kitaifa na kimataifa. Unajua Ebola imekuwepo Beni kuanzia tarehe mosi Agosti mwaka 2018. Radio Okapi kwa mara nyingine tena imekuwa zaidi ya sauti yetu.  Kuanzia suala la afya na katika magumu yote tunayotambua na  jamii yetuna vikundi vilivyojihami ambavyo vimekuwa vinatesa vikundi vinavyotoa  huduma, ni radio Okapi ambayo imekuwa kipaza sauti chetu.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter